Majaliwa achangisha fedha za mfuko wa utamaduni, Rais Magufuli kuchangia Sh100 milioni

Muktasari:

Mfuko wa Utamaduni kwa Wasanii Tanzania umeanzishwa ambapo Waziri Mkuu nchini humo, Kassim Majaliwa akiendesha harambee ya kuchangia fedha ambapo Rais wa Tanzania, John Magufuli akiahidi kutoa Sh100 milioni.

Dar es Salaam. Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa ameongeza harambee ya kuchangia kuanzishwa kwa mfuko wa utamaduni kwa wasanii kwa kutoa Sh5 milioni huku Rais wa Tanzania, John Magufuli akiahidi kutoa Sh100 milioni.

Kuanzishwa mfuko huo kumekuja kufuatia ombi la wasanii ili uwawezeshe katika uendeshaji wa shughuli za sanaa Tanzania walilolitoa leo Ijumaa Novemba 15, 2019 katika Kongamano la Sanaa na Mwalimu Nyerere lililofanyika jijini Dar es Salaam.

“Serikali ni sikivu imewasikia kuhusu mfuko wa utamaduni na utaundwa humu ndani. Tunaanza na meza kuu,” amesema Majaliwa

“Mfuko huu kwa wasanii ni muhimu sana, ni sisi wasanii hatukuwa tayari kuwa nao kwa sababu hatukujua tutaufanyia nini. Mkiusimamia vizuri mtaona manufaa yake, Serikali inaunga mkono kuwepo kwa mfuko huu,” amesema

Katika kuchangia, Majaliwa ameanza na Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai ambaye ametoa Sh5 milioni huku akiahidi Bunge litachangia Sh5 milioni.

Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Bashiru Ally amechangia Sh500,000, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole akichangia Sh500,000 wakati CCM kama chama kikichangia Sh4 milioni.

 

Mkuu wa Mkoa Wa Dar es Salaam, Paul Makonda ametoa ahadi ya kuchangia milioni tano, Waziri wa Vijana, Utamaduni na Michezo amemuwakilisha Rais wa Zanzibar, Ali Mohamed Shein atatoa milioni tano.

Wengine waliotoa ahadi ya kuchangia mfuko huo wa Utamaduni ni Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Sofia Mjema ambaye atatoa milioni moja na ameahidi kuwashawishi wakuu wa Wilaya zingine za Dar es Salaam kutoa milioni moja kila mtu. Wilaya hizo ni za Kinondoni, Temeke, Kigamboni, Ubungo.

Hata hivyo, msanii wa vichekesho Masanja Mkandamizaji naye ametoa ahadi ya Sh50, 000 kuchangia mfuko huo, aliyewahi kuwa waziri wa mambo ya ndani nchini Tanzania, Lawrence Masha ametoa ahadi ya milioni moja huku Msemaji Mkuu wa Serikali ya Tanzania, Dk Hassan Abasi atatoa milioni tatu.

Baada ya shughuli hiyo, Majaliwa amesema zaidi ya Sh140 milioni zimechangwa.