Majaliwa azindua mpango kabambe wa jiji la Dodoma

Thursday February 13 2020

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza wakati

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza wakati alipozindua Mpango Kabambe wa jiji la Dodoma kwenye ukumbi wa Hazina jijini Dodoma, Februari 13, 2020. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu) 

By Sharon Sauwa, Mwananchi [email protected]

Dodoma. Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa ameagiza mawaziri nchini kuanza ujenzi wa majengo ya kudumu ya wizara zao katika eneo la Mtumba jijini Dodoma.

Majaliwa ametoa agizo hilo leo Alhamisi Februari 13, 2020 wakati akizindua mpango kabambe wa Jiji la Dodoma.

“Sasa mnaweza kuanza ujenzi wa majengo ya wizara zenu ya kudumu,” amesema.

Pia,  ameitaka halmashauri ya Jiji la Dodoma kuongeza kasi ya upimaji wa viwanja na kuboresha miundombinu ya Jiji hilo.

Uzinduzi huo uliofanyika leo uliwashirikisha viongozi mbalimbali wakiwemo Spika wa Bunge, Job Ndugai, mawaziri, manaibu mawaziri na madiwani.

Mwenyekiti wa Mpango Kabambe huo, Profesa John Lupala amesema mchakato wa uandaaji wa mpango huo ulianza Oktoba mwaka juzi na kumalizika Desemba 2019.

Advertisement

Amesema wamefanya mikutano katika kata zote 41 za wilaya ya Dodoma Mjini kwa kuzingatia Sheria ya Mpango Miji inavyotaka.

Profesa Lupala amesema kuwa wamependekeza kuwepo kwa barabara za mpishano kwenye makutano ya barabara kubwa zote.

“Badala ya kujenga barabara wakati wananchi wameshajenga tulikubaliana na wenzetu wa Tanroad (Wakala wa Barabara Nchini) waanze kuyaainisha,” amesema.

Amesema kwa sababu ofisi ya Ikulu Chamwino imekatwa mara mbili walipendekeza kuwa upangaji unaweza kuingizwa kwenye mpango huo na utawala ukabakia kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino.

Amebainisha kuwa pendekezo jingine linahusu uendelezwaji wa majengo yaliyopo kandokando ya barabara kuu zinazoingia jijini Dodoma.

Amesema pia wametengeneza taswira katika eneo la Nzuguni ambalo litatatua changamoto ya msongamano wa watu na magari kutokana na eneo hilo kuwa na soko kuu, stendi ya mabasi yaendayo mkoani na kiwanja cha mpira.

Amesema katika eneo hilo la Nzuguni wamependekeza kuwepo kwa barabara mbili za juu za mpishano.

Kwa upande wa mji wa Serikali, Profesa Lupala amesema wamependekeza kuwepo masoko makubwa, kituo kikubwa cha mabasi, kwa barabara za mwendo wa kasi kwa ajili ya mabasi ya umma.

 

Advertisement