Maji bado tatizo Kigoma Ujiji, sababu zatajwa

Muktasari:

Ukosefu wa fedha umetajwa kuwa sababu ya kutokamilika kwa mradi wa maji wa Mgumile manispaa ya Kigoma Ujiji na kusababisha wananchi kukosa maji

Kigoma. Ukosefu wa fedha umetajwa kuwa sababu ya kutokamilika kwa mradi wa maji wa Mgumile manispaa ya Kigoma Ujiji na kusababisha wananchi kukosa maji.

Hayo yameelezwa  jana Jumapili  Agosti 25, 2019 na mhandisi wa maji manispaa ya Kigoma Ujiji, Leonard Watashe katika kikao cha wadau mbalimbali kujadili mradi wa uwazi na uwajibikaji katika sekta ya maji.

Amesema mradi huo ulisainiwa mwaka 2014 lakini haujatekelezwa kwa sababu ya ukosefu wa fedha.

Amebainisha kuwa baada ya kukosa fedha kutoka wizarani  kwa wakati huo, mkataba ulisitishwa na kuhuishwa mwaka  2017. Awali gharama za mradi zilikuwa Sh549 milioni.

Watashe amesema  baada ya kuanza utekelezaji ilibainika mradi una upungufu katika usanifu na kusahihishwa  jambo lililoongeza gharama hadi Sh736 milioni kutoka Sh549 milioni za awali.

“Juhudi za  kuwasiliana na wizara zilifanyika ili waweze kutuongezea fedha za mradi na Serikali ilikubali lakini mpaka sasa hatujapatiwa fedha,” amesema Watashe.