Majina wanafunzi watakaopata mkopo kutangazwa Oktoba 17

Muktasari:

Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) imesema Oktoba 15 na 17,  2019 yatatangazwa majina ya wanafunzi watakaonufaika na mkopo.

Dar es Salaam. Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) imesema Oktoba 15 na 17,  2019 yatatangazwa majina ya wanafunzi watakaonufaika na mkopo.

Hadi Oktoba 30, 2019  kabla ya vyuo kufunguliwa fedha za wanufaika hao zitakuwa zimefika vyuoni na bodi hiyo ina kiasi cha Sh125 bilioni.

Akizungumza na vyombo vya habari leo Jumatano Oktoba 9, 2019 mkurugenzi mtendaji wa bodi hiyo,  Abdul-Razaq Badru amesema majina ya wanafunzi waliopangiwa mikopo  yataanza kutoka tarehe hizo mbili.

“Fedha zipo Sh125 bilioni za robo ya kwanza ya mwaka tayari tunazo, kama chakula kimeiva kinasubiri walaji na kabla ya Oktoba 30 zitakuwa zimefika vyuoni mwao, yaani wakifungua vyuo wanazikuta, ”amesema Badru.

Akisisitiza suala hilo naibu Waziri wa Elimu nchini Tanzania, William Olenasha  amevitaka vyuo kuhakikisha wanafunzi wanapata fedha kwa wakati.

Olenasha aliyefanya ziara katika bodi hiyo leo amesema kumekuwa na malalamiko ya mikopo kufika vyuoni lakini kutowafikia walengwa kwa wakati.

“Hawa wanaochelewesha tutakula nao sahani moja kama fedha zipo bodi imezitoa kwa wakati nini kinachelesha kuwafikia walengwa, ”amesema Olenasha.

Waziri huyo pia aliwataka wanafunzi kufuata maelekezo wanayopewa kwa wakati ili kurahisisha mchakato wa kupatiwa fedha zao.

“Naviagiza vyuo vikuu kuwasilisha taarifa mapema kwenye bodi ya mikopo, kuna taarifa kuwa baadhi havijawasilisha  tena vipo vyuo vikubwa, hili si sawa,” amesema Olenasha.