Makonda: Mkapa alinipa nauli nikagombee UVCCM

Monday February 17 2020
pic makonda

Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amesema mwaka 2012 alipewa nauli na Rais mstaafu, Benjamin Mkapa kwenda mkoani Dodoma kugombea makamu mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM).

Akizungumza leo Jumatatu Februari 17, 2020 katika uzinduzi wa kipindi cha pili cha awamu ya tatu ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf) jijini Dar es Salaam, Makonda amesema naye ni alinufaika wa mfuko huo kwa sababu alipewa nauli na Mkapa ambaye ni mwanzilishi wa mfuko huo.

“Namshukuru sana mzee Mkapa kuona bado anaendelea kufanya kazi yake, naomba Rais Magufuli niseme mbele yako mfuko huu wa Tasaf nami nimenufaika nao, haikuwa moja kwa moja.”

“Lakini wakati naomba nafasi ya  makamu mwenyekiti wa vijana (UVCCM) Mkapa ndio aliyenipa nauli ya kwenda kuomba kura Dodoma. Kwa hiyo naimani ilikuwa sehemu ya huu mfuko, alikuwa na moyo,” amesema Makonda.

Makonda amesema wananchi kutoka mitaa 304 ya mkoa wa Dar es Salaam wamenufaika na mfuko huo.

“Wengi wamekuwa waaminifu kutumia kama maelekezo yalivyo, fedha hiyo imetumika kama mbegu na inatumika kuongeza chachu ya maendeleo kwa mtu mmoja, familia na Taifa,” amesema Makonda.

Advertisement

Katika hatua nyingine Makonda amewakumbusha wakati wa Mkoa wa Dar es Salaam kujiandikisha katika daftari la wapiga kura ili waweze kutumia haki yao ya msingi kuchagua viongozi wanaowataka katika uchaguzi mkuu ujao.

Advertisement