Makonda: Tuepuke ujuaji, tutaishinda corona

Friday March 20 2020
pic makonda

Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amesema amewaomba wakazi wa Jiji hilo kuepuka kuwa wajuaji wa kila jambo ili kuunusuru Mkoa huo na kuenea kwa maambukizi ya virusi vya corona.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Ijumaa Machi 20,2020, Makonda amesema kitendo cha kuwa mjuaji kwa maeneo ambayo hawajayasomea yanasababisha hofu na taharuki kwa wengine.

Amewasihi wananchi wafuate ushauri wa wataalamu ili kujikinga na virusi vya corona ambavyo vimeingia nchini na mpaka jana jioni Alhamisi watu sita walikuwa wamebainika kuwa na corona.

“Mkoa wangu wa Dar es Salaam ndiyo unaongoza kwa wajuaji, niwaombe watu wote mnaofahamu mnajua vitu ambavyo hamvijui msilete ujuaji katika tatizo la corona, ujuaji mmoja wapo ni kutokufuata masharti na mimi nataka mkoa huu watu wote tuwe salama ili tupate nafasi,” amesema Makonda

Amesema Serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali ikiwamo kuwapima watu wanaohisiwa kuwa na virusi vya corona, “wapo wengine wamekwenda kuchukuliwa vipimo na taarifa itatolewa kama ilivyotolewa kwa wengine.”

Makonda amesema wenyeviti wote wa mitaa na wajumbe wao wa serikali za mitaa wanao haki kimsingi kufahamu wageni wao kwenye mitaa wanayoiongoza ili kama kuna mgeni ameonyesha hizo dalili asaidie.

Advertisement

“Usalama siyo kulinda majambazi tu hata mlipuko wa magonjwa kama haya, msitumie nguvu wala vitisho kufahamu wageni walioingia katika mtaa yenu,” amesema  

Amesema kila mwenye nyumba aliyekuwa na mgonjwa mwenye dalili hizo msimfiche kwani anayefanya hivyo analeta madhara kwenye familia na kwa wengine.

Mkuu huyo wa mkoa amewaomba wananchi kuepuka mikusanyiko isiyokuwa ya lazima kama kwenda baa na kumbi za starehe akisema watulie majumbani na wafungulie muziki na kucheza makwao na pindi ugonjwa huo ukiondoka wananchi waendelee na shughuli zao kama kawaida.

Katika kuhakikisha vitakasa mikono na barakoa (maski) vinapatikana kwa wingi, Makonda amesema amezungumza na ubalozi wa China nchini ili uweze kusaidia na ubalozi huo umekubali.

Katika hatua nyingine, Makonda ametoa ombi kwa wizara ya fedha kuangalia jinsi inavyoweza kupunguza kodi kwa malighafi za kutengeneza vitakasa mikoni ili viweze kupatikana kwa bei nafuu.

Advertisement