Makonda atangaza siku tano ukaguzi bure wa magari Dar

Thursday December 05 2019
makondapic

Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ametangaza siku tano,  kuanzia Desemba 10 hadi 15, 2019  kwa wenye magari kufanya ukaguzi ili wasafiri salama kwenda mikoani kwa ajili ya mapumziko ya sikukuu za mwisho wa mwaka.

Makonda ametangaza ukaguzi huo leo Alhamisi Desemba 5, 2019 baada ya kukutana na wamiliki na mafundi gereji ambao walikubali  kufanya kazi hiyo bure ikiwa ni ofa ya mwisho wa mwaka.

Amesema ajali nyingi za barabarani zinatokana na wamiliki wa magari kutojenga tabia ya kufanya ukaguzi wa mara kwa mara ili kubaini kasoro.

"Kwa hiyo tutatangaza gereji zilizo tayari kwa kazi hii pelekeni magari yenu ili safari iwe salama," amesema Makonda.

Awali,  baadhi ya wamiliki na mafundi wa gereji walisema wapo tayari kufanya kazi hiyo kwa sababu watu wengi watajua changamoto za magari yao kabla ya kuanza safari.

"Tutawashauri kulingana na changamoto tutakazokutana nazo," amesema Elgius Mndale, fundi gereji kutoka wilayani Temeke.

Advertisement

Mkurugenzi wa Evolution Investment & General Supplies Ltd, Anthony Mganja amesema pamoja na kufanya ukaguzi huo, wapo tayari kutengeneza magari ya Serikali ya Mkoa wa Dar es Salaam  kwa kipindi cha miezi sita.

"Tunaunga mkono kazi za Rais John Magufuli za kuleta maendeleo, kwa hiyo pamoja na ukarabati wa magari ya Serikali tupo tayari kusaidia," amesema Mganja.


Advertisement