VIDEO: Makonda awaonya watendaji, asema anaanza kuwashughulikia

Wednesday September 25 2019

Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amesema katika kipindi cha uongozi wake hajawahi kutoa onyo kwa njia ya barua kwa kiongozi yeyote chini yake ndani ya mkoa huo, lakini sasa ataanza kuwashughulikia kutokana na hujuma anazofanyiwa.

Makonda ametoa kauli hiyo leo Jumatano Septemba 25, 2019 wakati wa mkutano wa kupokea na kuchambua miradi inayotekelezwa katika Jiji hilo kupitia ahadi za Ilani ya Chama cha Mapinduzi(CCM), iliyo na thamani ya takribani Sh3trilioni.

“Mie nimekuwa mkuu wa mkoa, sijawahi kuandika barua kumsema kiongozi yeyote, siyo mkuu wa wilaya, siyo mkurugenzi wala meya,” amesema Makonda.

“Sasa ninaanza kuwasema, kama mnavyopambana nyie kupitisha vimemo, mara ohh maelekezo yake hatumwelewi, mmepiga majungu muda mrefu sasa tutaanza kushughulikiana ili kila mmoja akae kwenye reli. Mie nawaita ofisini nawaambia jamani kwenye wilaya yako fanya hii nzuri,” amesema Makonda.

Makonda aliyepanda kuwa mkuu wa mkoa ndani ya mwaka mmoja baada ya kutumikia ukuu wa wilaya ya Kinondoni, amesema baadhi ya watendaji anaowashauri wamekuwa wabishi, hata kuonekana wakishindana naye licha ya kutumia mwongozo wa kazi.

“Aliyekuwa ananielewa haraka ni (Ali) Hapi tu,” amesema Makonda

Advertisement

Hapi alikuwa mkuu wa wilaya ya Kinondoni ambaye baadaye aliteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa.

Makonda amesema, “Mnanipinga, Rais (John Magufuli) kanipa nafasi ya kuwepo hapa kuwasimamia nyie. Nawaambieni hamtaki, sasa nasema uko chini yangu tu, haijalishi unanizidi miaka au nimekukuta serikalini, uko chini yangu tu. Tusifanye kazi ikawa ngumu.”

Advertisement