Malinzi, Mwesigwa walivyotoka gerezani

Muktasari:

Jana Jumatano Desemba 11, 2019 Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu iliwahukumu aliyekuwa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi na aliyekuwa katibu mkuu, Celestine Mwesigwa kifungo cha miaka miwili au kulipa faini.

Dar es Salaam. Jana Jumatano Desemba 11, 2019 Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu iliwahukumu aliyekuwa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi na aliyekuwa katibu mkuu, Celestine Mwesigwa kifungo cha miaka miwili au kulipa faini.

Malinzi alitakiwa kulipa faini ya Sh500,000 na Mwesigwa Sh1 milioni, faini ambazo kama wangeshinda kuzilipa wangetumia kifungo hicho cha miaka miwili kila mmoja.

Hukumu hiyo ilihitimisha safari ya miaka miwili ya kesi ya Malinzi na wenzake baada ya kupandishwa mahakamani kwa mara ya kwanza  Juni 29, 2017 wakikabiliwa na makosa mbalimbali.

Hata hivyo, wawili hao walirudishwa gerezani ili kukamilisha taratibu za hukumu hiyo leo Alhamisi Desemba 12, 2019.

Wakiwa na nyuso za matumaini, ndugu, jamaa na marafiki wachache wa Jamal Malinzi na Celestine Mwesigwa leo walitumia saa 2:14 kukamilisha taratibu na kurejea uraiani na viongozi hao wa zamani wa mpira waliokaa rumande kwenye gereza la mahabusu Keko kwa siku 897.

Malinzi na Mwesigwa wametoka gerezani saa 5.14 asubuhi na kupokewa ndugu hao  wasiozidi wanane waliwasili gerezani hapo saa 3.00 asubuhi wakiwa na risiti ya malipo ya faini wakiongozwa na mwanasheria wa watuhumiwa, Lucy Ngongoseke na mmoja wa ndugu wa Malinzi aliyejitambulisha kwa jina moja la Julius huku wengine watano wakisubiri nje ya uzio wa gereza.

Wakati Malinzi na Mwesigwa wakihukumiwa, mahakama hiyo iliwaachia huru aliyekuwa mhasibu wa TFF, Nsiande Mwanga na karafi Flora Rauya baada ya upande wa mashtaka kushindwa kuthibitisha mashtaka dhidi yao.

Malinzi alikutwa na hatia ya kughushi muhtasari wa kamati ya utendaji ya TFF huku Mwesigwa akikutwa na hatia ya makosa mawili, kwa kutengeneza na kuandaa nyaraka za uongo huku akijua kufanya hivyo ni kosa la kisheria.

Kwa habari zaidi kuhusu Malinzi na Mwesigwa walivyotoka gerezani  soma gazeti la Mwananchi la kesho Ijumaa Desemba 13, 2019.