Mama wa bilionea Msuya aomba suluhu nje ya mahakama

Muktasari:

Ndeshukurwa Sikawa ambaye ni mama mzazi wa marehemu, bilionea Erasto Msuya ameiomba Mahakama Kuu Kanda ya Arusha nchini Tanzania muda wa kusaka suluhu ya kesi ya kugombea usimamizi wa mirathi za mwanaye.

Arusha. Ndeshukurwa Sikawa ambaye ni mama mzazi wa marehemu, bilionea Erasto Msuya ameiomba Mahakama Kuu Kanda ya Arusha nchini Tanzania muda wa kusaka suluhu ya kesi ya kugombea usimamizi wa mirathi za mwanaye.

Ameeleza hayo leo Jumanne Januari 28, 2020, kubainisha kuwa anataka kutafuta suluhu hiyo nje ya mahakama.

Sikawa alifungua kesi hiyo akitaka mjane wa bilionea huyo, Miriam Mrita kuondolewa kusimamia mirathi.

Maombi yake hayo yamewasilishwa na wakili wake, Fadhili Nangawe mbele ya hakimu Yohane Masala anayesikiliza kesi hiyo.

Wakili Nangawe aliomba kabla ya  kusomwa uamuzi, wapewe muda ya kufanya mazungumzo nje ya Mahakama.

Desemba 13, mahakama hiyo ilisema leo ndio itatoa hukumu ya kugombea usimamizi wa mirathi ya mali za marehemu.

Jaji Masare amekubali maombi hayo na kutoa miezi miwili kesi hiyo kusuluhishwa nje ya mahakama.

Wakili Shilinde Mgalula, anayemtetea mjane wa bilionea Msuya alieleza kukubaliana na maombi hayo.

Katika kesi hiyo namba 66/2019 mama wa bilionea huyo alitaka Mrita kuondolewa kuwa msimamizi wa mirathi hiyo akimtuhumu kuanza kuuza mali za marehemu mumewe.

Miriam kupitia wakili wake, Shilinde Ngalula aliweka pingamizi kuhusu shauri hilo kwa hoja kuwa tayari limetupwa mara mbili na Mahakama Kuu kwa kuwa lilikuwa tayari limeshafunguliwa.

Bilionea Msuya aliuawa kwa kupigwa risasi Agosti 7, 2013 na ameacha nyumba za kifahari tano, magari, hoteli mbili za kitalii, viwanja na mgodi wa madini ya Tanzanite.