VIDEO: Mambo sita anayojutia Mzee Mkapa

Wednesday November 13 2019

 

By Waandishi Wetu, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Rais Benjamin Mkapa aliyeongoza Taifa mwaka 1995 hadi 2005 ameeleza mambo sita ambayo anaona yametia doa kipindi cha uongozi wake wa miaka 10, akitaja mojawapo kuwa ni mauaji ya watu 22 kisiwani Pemba, Zanzibar.

Maneno hayo ya Mkapa yamo katika kitabu chake cha “My Life, My Purpose (Maisha Yangu, Kusudi Langu)” ambacho kilizinduliwa jana na Rais John Magufuli katika hafla iliyofanyika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.

Katika kitabu hicho chenye kurasa 319, Mkapa, ambaye jana alitimiza umri wa miaka 81, alizungumzia, mambo chanya na hasi ambayo yalitokea kipindi hicho.

“Baadhi ya matukio yalikuwa ni magumu ambayo yamekuwa na matokeo hasi na chanya kwenye maendeleo yetu,” alisema katika hotuba yake iliyojikita kueleza sababu za kuandika kitabu hicho na baadhi ya mambo aliyoandika.

“Baadhi ya matukio lazima nikiri yalikuwa ni magumu kuyahadithia na kuyaweka kwenye maandishi, lakini sikutaka kuyaacha kwa kuwa naamini kiongozi wa kweli anajengwa na matukio yote; hasi na chanya kwenye maisha yake binafsi na kwenye maisha yake kama kiongozi wa umma.

“Kama kiongozi, mara nyingi unajaribu kuangalia uwiano bora wa vipaumbele kulingana na taarifa unazokuwa umepewa kwa wakati ule ambazo si wananchi wengi wanakuwanazo, lakini kama binadamu wakati mwingine tunafanya makosa.”

Advertisement

Mkapa alitaja mambo hayo kuwa ni mauaji ya wananchi 22 wa kisiwani Pemba wakati wa vurugu za uchaguzi, ununuzi wa rada, kuchukua mkopo kwa anuani ya Ikulu, sakata la uchukuaji fedha kutoka Akaunti ya malipo ya Madeni ya Nje (Epa), ubinafsishaji na kuuzwa kwa nyumba za Serikali.

Alipata mshtuko

Kuhusu mauaji ya wafuasi 22 wa CUF, Mkapa ameeleza kujutia tukio hilo ambalo anasema liliwafanya viongozi wa chama hicho wamtangaze kuwa hakujali kilichotokea.

Mkapa, ambaye anasema alikuwa Davos, Uswisi wakati mauaji hayo yanatokea, anakiri kuwa yalimpa wakati mgumu na kukumbushia alipohojiwa katika kipindi cha Hard Talk cha BBC na Tim Sebastian.

“Maswali yake yalikuwa ya kukasirisha. Alishika hoja kuwa Serikali iliamuru kwa makusudi mauaji ya waandamanaji,” ameandika Mkapa katika kitabu hicho.

Anasema alikasirika na kumuuliza yeye ni nani hadi aulize masuala ya mawasiliano kati ya Serikali na polisi kwa njia hiyo. Anasema alikosolewa kwa jinsi alivyomjibu mwandishi huyo.

“Siku hizo, sisi marais wa Afrika hatukuwa tumezoea kuzungumza na mtu yeyote kwa njia hiyo. Siku hizi, aina hii ya mahojiano ya kushambuliana ni ya kawaida,” ameandika.

Alisema kutokana na hilo, CUF ilimsakama kutaka kuonyesha kuwa hakujali na kwamba ni kiburi chake cha kawaida.

“Bila wasiwasi, nilijutia mauaji haya. Najutia hadi leo, lakini nadhani kuwa kuna mtazamo usio sahihi wa watu wa Magharibi kuwa jamii zote zinafanana-- kitu ambacho si sahihi,” ameandika.

Anasema baada ya tukio hilo alirejea nchini na kuanza kutafuta suluhisho.

Ubinafsishaji

Mkapa pia ameelezea mpango wa ubinafsishaji wa mashirika ya umma ambao umemfanya awe anakosolewa kila mara kutokana na kuonekana haukufanyika vizuri.

Anakiri kuwa malalamiko makubwa ni namna yalivyouzwa kwa bei ya chini na wageni wakipewa kipaumbele.

Alitoa mfano wa uamuzi wa kuileta kampuni ya Net Group Solution ya umeme kutoka Afrika Kusini kulivyochafua hali ya hewa kutokana na ukweli kuwa kulikuwa na shemeji yake kwenye menejimenti yake.

Net Group ililetwa nchini kwa ajili ya kusimamia Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) ili liweze kujiendesha kwa faida.

Pia kitendo cha kuutoa mgodi wa makaa ya mawe wa Kiwira mkoani Mbeya kwa baba mkwe wa mwanae.

Mkapa anaandika kuwa watu walichukulia suala hilo kwa mtazamo hasi na matokeo yake Serikali ilichukua mgodi ule mwaka 2008 na hadi leo haujaendelezwa.

Epa

Sakata la madai ya ufisadi wa zaidi ya Sh133 bilioni kwenye akaunti ya Epa iliyokuwa Benki Kuu (BoT) pia limetajwa kuwa mwiba mwingine kwa Mkapa.

Kashfa hiyo iliibuka bungeni mwaka 2008 ikihusisha baadhi ya vigogo wa benki hiyo, maofisa wa Serikali pamoja na wafanyabiashara maarufu walioghushi barua za kuonyesha kuwa wamerithishwa madeni na kampuni za nje.

Mkapa anaeleza kuwa alishauriwa na gavana wa wakati huo, marehemu David Balali, ambaye alimueleza kuwa kuna wafanyabiashara walikuwa tayari kununua deni hilo na baadaye kuchangia kampeni za CCM.

“Wahuni walitumia uaminifu wangu kwa chama kunishawishi. Ninajisikia kuwa nilisalitiwa na kutumika. Ukweli ni kwamba sikufaidikia chochote na fedha hizo,” anasema Mkapa.

Mkapa pia ameutaja mpango wa kuuza nyumba za Serikali kuwa ni miongoni mwa dosari katika uongozi wake akisema kipindi hicho yaliibuka malalamiko mengi ya utaratibu huo kuendeshwa kwa upendeleo, huku baadhi ya nyumba zikiuzwa kwa watu wasiohusika.

Serikali ilikuwa imeelekeza nyumba hizo kuuzwa kwa watumishi wa umma na sio watu binafsi.

Suala la ununuzi wa rada kwabei kubwa kutoka kampuni ya Bae System ya Uingereza mwaka 2002 pia amelitaja kuwa ni dosari nyingine.

Uingereza ndiyo iliyobaini mchezo huo na kufanya uchunguzi uliosababisha Novemba 2013 Tanzania irejeshewe pauni 29.5 za Kiingereza (sawa na Sh73 bilioni) ambazo zililetwa kwa njia ya vifaa vya elimu.

Kutumia anuani ya Ikulu kukopa

Suala lililoibuka baada ya Mkapa kuondoka madarakani ni kuchukua mkopo benki kwa kutumia kampuni ambayo ilikuwa na anwani ya Ikulu. “Ni kweli nikiwa Ikulu nilichukua mkopo kwa masharti ya kawaida ya biashara na nilipotoka madarakani nilikuwa nimemaliza kulipa mkopo kwa kutumia mshahara na mafao yangu,” anasema Mkapa.

Mambo chanya ya utawala

Pamoja na kasoro hizo, Mkapa ametaja mambo mazuri aliyofanya katika kipindi chake ikiwa ni pamoja na kuanzisha Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf) mwaka 1999.

“Tasaf kwa kweli ninahesabu ni high point (mafanikio ya juu) katika utawala wangu,” alisema Mkapa, ambaye anadai kupingwa na mawaziri wake.

Ametaja jambo jingine kuwa ni kupanda kwa ukusanyaji mapato. Anasema wakati anaingia madarakani, Serikali ilikuwa inakusanya dola 612,000 za Kimarekani (Sh1.3 bilioni) kwa mwezi, lakini hadi anaondoka walikuwa wanakusanya dola 1.7 milioni (Sh3.8 bilioni).

Suala jingine ni kuanzisha ofisi za mawakala mbalimbali ambazo zimesaidia utekelezaji wa shughuli za Serikali.

Taasisi hizo ni kama Mamlaka ya Mapato (TRA), Mfuko wa Bima ya Afya (NHIF), Barabara (Tanroads) na Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA).

Pia amesema katika kipindi chake riba ya mikopo ya benki ilishuka kutoka asilimia 36 hadi asilimia 15 mwaka 2005 wakati anatoka madarakani.

Pia amesema mwaka 1995 alikuta akiba fedha ya kigeni ilikuwa inayotosha kuendesha nchi kwa mwezi mmoja na nusu, lakini alipoachia ngazi aliacha akiba ya miezi mitano.


Advertisement