KASHFA: Maswali yasiyo na majibu wizi wa kompyuta ofisi ya DPP

Saturday October 19 2019

 

By Elizabeth Edward, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Habari kuwa wezi wameingia ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) na kufanikiwa kuiba kompyuta, zinaaminisha wasomi kuwa kuna uzembe umefanyika unaoacha maswali mengi.

Habari hizo zilisambaa juzi jioni na kuripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari jana na kamanda wa polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa alinukuliwa akisema amepata taarifa za wizi huo.

Imeripotiwa kuwa wizi huo ulifanyika Jumanne, wiki ambayo ofisi ya DPP imekuwa ikishughulikia washtakiwa wa uhujumu uchumi wanaofanya mazungumzo na DPP kukiri na kukubaliana malipo ya kurejesha.

Hofu ya wachambuzi wengi ni uwezekano wa wizi huo kukumba nyaraka muhimu za ofisi hiyo ya mwendesha mashtaka wa umma katika kipindi cha majadiliano ya kesi za mabilioni ya fedha.

“Ni wizi wa kawaida lakini utasababisha mshangao mkubwa kama kweli taarifa zilizopo kwenye kompyuta hizo zitakuwa zimepotea,” alisema mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Anna Henga.

Hata hivyo, alisema Serikali ina wataalamu wa Tehama na hivyo haiwezekani taarifa muhimu ziwe kwenye kompyuta moja.

Advertisement

Ugumu wa suala hilo pia ulionekana kwa Dk Onesmo Kyauke aliyesema mazingira ya wizi huo bado hayaeleweki.

“Pale kuna ulinzi, wizi unatokeaje? Kwanza kompyuta zilizoibiwa ni ngapi na kweli taarifa zipo kwenye kompyuta moja tu?” alihoji Dk Kyauke.

Maswali kama hayo alikuwa nayo mwanaharakati Kijo Bisimba.

“Nimeshangaa kwanza hiyo ofisi inakosaje usalama kiasi cha kompyuta hizo kuibiwa. Najiuliza kuibiwa kwake ina maana ndiyo nyaraka zipotee na hizo nyaraka zinamnufaisha nani kwa kifupi ninajiuliza maswali mengi,” alisema mkurugenzi huyo wa zamani wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu.

Naye mchambuzi wa masuala ya siasa, Profesa Gaudence Mpangala alisema kama kweli tukio hilo limetokea katika ofisi nyeti ya Serikali, kuna uzembe mkubwa.

“Ile ofisi ni nyeti lazima ilindwe. Swali linakuja mpaka kompyuta zinaibiwa ni wazi hakukuwa na ulinzi. Sasa walinzi walikuwa wapi na waliohusika kufanya huo wizi ni akina nani na walifanya kwa lengo lipi,” alihoji Mpangala.

Alisema kama kweli itathibitika kuwa wizi huo umetokea, basi DPP mwenyewe anapaswa kuanza kuwajibika kwa kuruhusu uzembe wa aina hiyo.

Alipotafutwa kuzungumzia suala hilo, msemaji wa Serikali, Dk Hassan Abbasi alijibu: “Mimi sisemei taasisi, waulizeni wenyewe ofisi ya DPP wazungumzie wenyewe na kama ni tukio la jinai waulizeni polisi. Mimi ni msemaji wa serikali kwa masuala ya kitaifa sio kuzungumzia taasisi.”

Naye Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Simon Sirro hakutaka kuzungumzia suala hilo alipoulizwa na Mwananchi, badala yake akasema aulizwe Mambosasa ambaye msaidizi wake alieleza kuwa alikuwa kwenye kikao.

Advertisement