Matokeo darasa la nne, kidato cha pili na nne haya hapa
Katibu Mtendaji wa Necta Dk Charles Msonde akizungumza na waandishi wa habari alipokuwa akitangaza matokeo ya mtihani wa taifa wa darasa la nne, kitado cha pili na kidato cha nne jijini Dar es Salaam jana
Muktasari:
Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani ya Taifa (Necta) nchini Tanzania, Dk Charles Msonde leo Alhamisi ametangaza matokeo ya upimaji kwa darasa la nne, kidato cha pili pamoja na mtihani wa kuhitimu kidato cha nne mwaka 2019.
Dar es Salaam. Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) nchini Tanzania limetangaza matokeo ya mtihani wa upimaji darasa la nne, kidato cha pili na kidato cha nne.
Katika matokeo hayo yaliyotangazwa leo Alhamisi Januari 9, 2020 na Katibu Mtendaji wa Necta, Dk Charles Msonde amesema ufaulu katika mtihani wa upimaji wa darasa la nne umeongezeka kwa asilimia 26.21.
Jumla ya watahiniwa 1,531,120 kati ya wanafunzi 1,665, 863 wamepata alama A,B,C na D ikilinganishwa na wanafunzi 1,213, 132 waliofaulu mwaka 2018.
Katika mtihani wa upimaji kidato cha pili, wanafunzi 514,251 sawa na asilimia 90.04 kati ya wanafunzi 571,137 wamefanya vizuri katika mtihani huo na kuwawezesha kuingia kidato cha tatu.
Dk Msonde amesema mtihani wa kidato cha nne jumla ya watahiniwa 340,914 sawa na asilimia 80.65 ya watahiniwa 422,722 wameefaulu mitihani yao.
Watahiniwa hao ni sawa na ongezeko la asilimia 1.38 ikilinganishwa na watahiniwa 284,126 sawa na asilimia 79.27 waliofaulu mtihani huo mwaka 2018.