Mbowe, vigogo Chadema kuanza kujitetea Septemba 17

Muktasari:

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imewakuta na kesi ya kujibu viongozi tisa wa Chadema akiwemo mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe na wataanza kujitetea Septemba 17, 2019.

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imewakuta na kesi ya kujibu viongozi tisa wa Chadema akiwemo mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe na wataanza kujitetea Septemba 17, 2019.

Mbowe na viongozi wengine wanane wa chama hicho wakiwemo wabunge sita wanakabiliwa na kesi ya jinai namba 112/2018 yenye mashtaka 13 yakiwemo ya uchochezi.

Uamuzi huo umetolewa leo Alhamisi Septemba 12, 2019 na Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Thomas Simba baada ya upande wa mashtaka kufunga ushahidi wao.

Hakimu Simba amesema amepitia ushahidi wa mashahidi nane wa upande wa mashtaka pamoja na vielelezo,  kujiridhisha kuwa washtakiwa wote wana kesi ya kujibu.

“Baada ya kupitia ushahidi uliotolewa mahakama hapa na upande wa mashtaka, nimejiridhisha kuwa washtakiwa wote wana kesi ya kujibu wanatakiwa kujitetea,” amesema Hakimu Simba.

Baada ya kueleza hayo Hakimu Simba ameahirisha kesi hiyo hadi Septemba 17, 18 na 19,  2019 na washtakiwa wataendelea kuwa nje kwa dhamana.

Awali, wakili wa Serikali mkuu, Faraja Nchimbi alieleza mahakama hiyo kuwa upande wa mashtaka wamefunga ushahidi wao.

Tayari mashahidi wanane wa upande wa mashtaka wameshatoa ushahidi wao dhidi ya washtakiwa hao.

Miongoni mwa mashahidi hao ni  mkuu wa upelelezi kutoka Wilaya ya Kipolisi ya Mbagala, Bernard Nyambari(42), ambaye alieleza mahakama hiyo kuwa  hotuba zilizotolewa na viongozi wa Chadema katika mkutano wa kufunga kampeni ya uchaguzi mdogo wa ubunge Kinondoni, zilizofanyika katika viwanja vya Buibui ndio chanzo cha wananchi kuandamana.

Amedai akiwa mpelelezi wa kesi hiyo, uchunguzi waliofanya walibaini kuwa hotuba hizo ndio chanzo wananchi  na viongozi hao kufanya maandamano.

Washtakiwa wengine ni mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko; Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa; Naibu Katibu Mkuu Taifa-Zanzibar, Salum Mwalimu; Mbunge wa Kibamba, John Mnyika; Mbunge wa Kawe, Halima Mdee; Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche; Mbunge wa Bunda Mjini, Ester Bulaya na katibu mkuu wa chama hicho, Dk Vicent Mashinji.