VIDEO: Mbowe, wenzake wakutwa na kesi ya kujibu

Thursday September 12 2019

 

By Hadija Jumanne, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imewakuta na kesi ya kujibu viongozi tisa wa Chadema akiwemo mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe.

Mbowe na viongozi wengine wanane wa chama hicho wakiwemo wabunge sita wanakabiliwa na kesi ya jinai namba 112/2018 yenye mashtaka 13 yakiwemo ya uchochezi.

Uamuzi huo umetolewa leo Alhamisi Septemba 12, 2019 na Hakimu Mkazi Mkuu wa mahakama hiyo, Thomas Simba baada ya upande wa mashtaka kufunga ushahidi wao.

Washtakiwa wengine ni mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko; Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa; Naibu Katibu Mkuu Taifa-Zanzibar, Salum Mwalimu; Mbunge wa Kibamba, John Mnyika; Mbunge wa Kawe, Halima Mdee; Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche; Mbunge wa Bunda Mjini, Ester Bulaya na katibu mkuu wa chama hicho, Dk Vicent Mashinji.

Jana katika kesi hiyo Mkuu wa Upelelezi wilaya ya Kipolisi Mbagala, Bernard Nyambari alitoa ushahidi na kuieleza mahakama hiyo kuwa taarifa za kifo cha aliyekuwa mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwiline zinaonyesha alikufa akiwa hospitali ya Mwananyamala akipatiwa matibabu.

Alisema Akwilina alipata jeraha kichwani lililosababishwa na risasi, lakini hafahamu aliyempiga risasi mwanafunzi huyo.

Advertisement

Endelea kufuatilia Mwananchi kwa taarifa zaidi

Advertisement