Mbowe aieleza mahakama Chadema itakavyoshinda uchaguzi

Muktasari:

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Freeman Mbowe ametoa utetezi wake leo Ijumaa ambapo ameieleza mahakama jinsi chama hicho kitakavyoshinda uchaguzi na kuongoza Serikali ya Tanzania.

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania cha Chadema, Freeman Mbowe amesema chama hicho hakina dhamira ya kushika madaraka kwa kutumia nguvu au kuhamasisha chuki.

Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni nchini Tanzania amesema hayo leo Ijumaa Novemba 29, 2019 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam alipokuwa akihojiwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Faraji Nchimbi.

Wakili huyo amemuuliza Mbowe ni sera ya Chadema kuhamasisha vurugu, kuhamasisha watu kutembea na silaha barabarani, chuki kwa jamii na uvunjifu wa nchi Mbowe alijibu siyo sahihi.

Nchimbi alimuuliza Mbowe ni sahihi katika mazingira hayo naomba ifahamishe mahakama ibara na kifungu gani ndani ya katiba na sheria kinachoruhusu mtu au chama cha siasa kuchukua nchi kwa kumwaga damu akajibu kuwa hajui.

Pia, alimuuliza katika  miaka 15 ya ubunge hakuwahi kukutana na kifungu au ibara ya sheria na katiba inayomruhusu mtu au chama kuchukua madaraka kwa kupitia utaratibu wa kubeba majeneza, Mbowe alijibu hajui

Mbowe akiongozwa na Wakili wake wa utetezi, Peter Kibatala aliieleza mahakama hiyo kuwa  chama hicho kinakusudia kuchukua madaraka kwa kupitia sanduku la kura na siyo kushika madaraka kwa kutumia nguvu ikiwemo, kuhamasisha chuki, vurugu na kuhamasisha watu kutembea na silaha barabarani.

Mbowe amemaliza utetezi wake na sasa Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa anatoa utetezi wake.

Mbali na Mbowe, washtakiwa wengine ni Katibu Mkuu, Dk Vicent Mashinji, manaibu katibu wakuu, John Mnyika (Bara) na Salum Mwalimu (Zanzibar) na mbunge Tarime John Heche.

Wengine ni mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa; mweka hazina wa Baraza la Wanawake (Bawacha), Esther Matiko; mbunge wa Kawe, Halima Mdee na mbunge wa Bunda Mjibi, Ester Bulaya

Washitakiwa hao wanakabiliwa na mashitaka 13 likiwemo la kula njama, ambapo wote wanadaiwa, Februari 1 na 16, 2018, Dar es Salaam walikula njama ya kutenda kosa la kufanya mkusanyiko usio halali na kukiuka tamko la kutawanyika.