Mbowe na familia yake wajitenga wakisubiri majibu ya vipimo vya corona

Thursday March 26 2020

 

By Exaud Mtei, Mwananchi

Dar es salaam. Mwenyekiti wa Chadema ambaye pia ni kiongozi wa kambi rasmi ya upinzani Bungeni, Freeman Mbowe ameamua kujiweka karantini na familia yake baada ya mtoto wake kukutwa na virusi vya corona.


Juzi Katika taarifa yake kwa umma, Mbowe alieleza kuwa  mtoto wake aitwaye Dudley amethibitika kupatikana na virusi vya corona baada ya kupata homa za vipindi, kuumwa kichwa mfululizo na kukohoa kwa siku tano.


Akizungumza jana machi 25. 2020  na Clouds FM katika kipindi cha Jahazi, Mbowe amesema baada ya taarifa hizo ameamua kujitenga peke yake nyumbani Dodoma ambapo anaendelea na shughuli zake huku akisubiri majibu ya vipimo alivyofanya ili kuthibitisha kama amepata virusi hivyo au hakupata.


Vilevile, Mbowe amesema mbali na yeye kujitenga lakini pia familia yake ambayo ilikuwa karibu na mtoto ambaye amekutwa na virusi hivyo nao wamejitenga kwa siku 14 kwa lengo la kuona kama wamepata virusi hivyo


“Nipo Dodoma lakini nimeamua kwenda kwenye self-Isolation kwa sababu ikishasemekana kuwa familia yako ina ugonjwa huo kila mtu anakuangalia kwa jicho la hofu, unaingiza hofu katika jamii hivyo nimeamua kujitenga kukaa nyumbani na kufanyia kazi zangu nyumbani nasubiri majibu yangu” ameeleza Mbowe


Mbowe amesema tangu akutane na mwanaye huyo mwenye virusi hivyo ni zaidi ya siku 12 ambao ni muda mrefu lakini baada ya kutoka nyumbani alitembelea maeneo mbalimbali na kukutana na watu wengi ambapo amesema ni jambo la kumuomba Mungu awe hajapata virusi hivyo ili na watu aliokutana nao wawe salama.

Advertisement


Mbowe ameongeza kuwa suala la ugonjwa wa corona ni la kitaifa ambalo linahitaji mkakati wa pamoja wa kukabiliana nalo ikiwa ni pamoja na kuundwa kuwa kikosi kazi maalumu kwa ajili ya mapambano hayo

Advertisement