VIDEO: Mbunge wa Ndanda atangaza kugombea uenyekiti Chadema

Mtwara. Zikiwa zimebaki siku 72 Chadema kufanya uchaguzi mkuu wa viongozi wa kitaifa, Cecil Mwambe ametangaza kuwania uenyekiti.

Mbunge huyo wa Chadema wa Jimbo la Ndanda amepanga kuchuana na mwenyekiti wa sasa, Freeman Mbowe ambaye hata hivyo bado hajasema lolote kuhusu kugombea nafasi hiyo.

Mwambe anakuwa mwanachama wa kwanza wa chama hicho kikuu cha upinzani kutangaza nia yake.

Chadema imepanga kufanya uchaguzi wake mkuu Desemba 18, mwaka huu.

Bado haijafahamika kama Mbowe aliyeanza kukiongoza chama hicho mwaka 2004 akirithi nafasi ya Bob Makani (sasa marehemu) kama atagombea au vinginevyo.

Uongozi wa Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ulimalizika Septemba 14 na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ilitoa siku saba zinazomalizika leo saa 9.30 alasiri wawe wamewasilisha maelezo kwa nini hawajafanya uchaguzi.

Mbowe anayeelezwa kuwa ni mwanamikakati mahiri ndani ya chama hicho, alichaguliwa kwa mara ya tatu Septemba 15 mwaka 2014 kwa kura 789 sawa na asilimia 97.3 na kumshinda mpinzani wake Gambaranyera Mongateo aliyepata kura 20 sawa na asilimia 2.5.

Kwa habari Zaidi usikose Gazeti la Mwananchi Oktoba 7,2019. Pamoja na kutizama video iliyoambatanishwa hapa.