Mbunge wa tano CUF ahamia CCM

Muktasari:

Mbunge wa Wawi (CUF) Mkoa wa Kusini Pemba, Ahmed Juma Ngwali amejivua uanachama wa chama hicho na kuhamia CCM.

Unguja. Mbunge wa Wawi (CUF) Mkoa wa Kusini Pemba, Ahmed Juma Ngwali amejivua uanachama wa chama hicho na kuhamia CCM.

Ngwali ametangaza uamuzi huo leo Jumatatu Machi 2, 2020 mbele ya Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole ambaye yupo Zanzibar katika ziara ya kukagua utekelezaji wa Ilani ya CCM Wilaya za kisiwani Pemba.

Mbunge huyo amesema anajiunga CCM kwa sababu chama hicho tawala kinapeleka maendeleo kwa wananchi.

Ngwali anaungana na wabunge wengine wanne wa CUF waliojiunga CCM ambao ni Maulid Mtulia (Kinondoni), Ahmed Katani (Tandahimba), Abdallah Mtolea (Temeke) na Zuberi Kuchauka (Liwale).

Katika maelezo yake amesema CCM imekuwa ikifanya mambo mengi mazuri kuleta maendeleo ya wananchi  bila ya ubaguzi wa vyama.

Amebainisha kuwa yupo tayari kukosa marupurupu, mshahara na kiinua mgongo, “nimeamua kuachana na kila kitu ili kujiunga na CCM kwani ndio chama kinachofikisha maendeleo ya kweli kwa wananchi wake.”

Amesema kabla ya kuchukua uamuzi huo  alianza kuungana na CCM kwa kutoa huduma mbalimbali kwa wananchi, ikiwamo kusaidia ujenzi wa kituo cha afya na mambo mengine ya kijamii, “mambo ambayo ndio yalinipa  nguvu ya kuona CCM wapo pamoja nami, ni lazima kuwa pamoja nao kwa kujiunga nao.”

Polepole amesema alichokifanya Ngwali ni haki yake ya msingi, “nilipofika kituo cha afya kuangalia maendeleo ya kituo hicho, nilipata sifa sana kwa watu na viongozi kuwa kuna Mbunge anasaidia sana maendeleo ya kuunga mkono juhudi za wananchi, nikauliza Mbunge huyo anatoka chama gani, nikaambiwa anatokea Chama cha Madevu, nikatamani kumuona, lakini hapa kumbe amekuja kujipokea yeye, nimefurahi sana.”