Mdee ahojiwa kwa tuhuma za kumiliki vifaa vya kunasa sauti

Mgombea ubunge Kawe (Chadema), Halima Mdee

Muktasari:

Mgombea ubunge Kawe (Chadema), Halima Mdee jana alikamatwa na jeshi la polisi kituo cha Mbweni na kuhojiwa kwa tuhuma za kumiliki vifaa vya kunasia sauti kinyume na sheria za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).

Dar ea Salaam. Mgombea ubunge Kawe (Chadema), Halima Mdee jana Ijumaa Oktoba 23,2020 alikamatwa na jeshi la polisi kituo cha Mbweni na kuhojiwa kwa tuhuma za kumiliki vifaa vya kunasia sauti kinyume na sheria za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni Edwrd Bukombe alipotafutwa na gazeti hili kutolea ufafanuzi tukio hilo alisema hadi saa 1:20 jioni mgombea huyo alikuwa nje lakini akisisitiza kuwa hajawasiliana na waliomhoji, akiahidi kuwa atakapowasiliana nao atatoa ufafanuzi zaidi muda ambao wakili wa Mdee, Edson Kilatu alisema mgombea huyo muda huo alikuwa akitoa maelezo kituo cha polisi.

Hata hivyo jana saa 3 usiku Kilatu alisema Mdee aliachiwa kwa dhamana baada ya  kuchukuliwa maelezo na kutakiwa kuripoti polisi atakapohitajika.

Awali, Kilatu alisema Mdee alishikiliwa kituoni hapo baada kwenda kuripoti tukio la watu wanaomuwinda kutaka kupanga kwenye nyumba iliyopo jirani.

Alisema baada ya Mdee kushikiliwa na jeshi la polisi lilifanya upekuzi nyumbani kwake kwa zaidi ya saa moja na kuondoka na kompyuta mpakato moja.

“Baada ya kwenda kuripoti na kuandika maelezo ndipo polisi walipokuja na hoja ya kumiliki vifaa vya mawasiliano kinyume na sheria za TCRA ambapo baada ya kufanya upekuzi wameondoka nae na kurudi kituoni,”alisema Wakili Kilatu.

Meneja kampeni wa Mdee, Felista Njau alipotafutwa na gazeti hili alisema asubuhi mgombea huyo alienda kutoa taarifa kituo cha polisi Mbweni kuwa kuna magari yanayomfuatilia yakiwa na namba tofauti.

Alisema baada ya kufika kituoni hapo aliwekwa chini ya ulinzi na kuelezwa kuwa kuna jalada lake kituoni hapo nakutakiwa kwenda kufanyiwa upekuzi nyumbani kwake.

Juzi katika ukurasa wake wa Twitter,Mdee aliandika “Kesho nitaripoti Polisi…,kuna watu wananifuatilia nyumbani kwangu, wanaongeza dau kwa nyumba ya jirani yangu (ghorofa ambalo halijaisha) ili waweze kukodi chumba ili wafanye yao ,nilisema juzi naona hamjakoma leo mmekuja tena nakuongeza dau. Tusilaumiane.”