Membe, Dk Bashiru ngoma bado nzito

Muktasari:

Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally akiwa Bukombe mkoani Geita Jumamosi amesema anahitaji kukutana na mwanachama wa chama hicho, Bernard Membe ofisini kwake pasina kuwapo kwa masharti yoyote

Dar es Salaam. Kitendo cha Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally kumtuhumu hadharani Bernard Membe kuwa anakwamisha mkakati wa urais 2020 kimeibua mjadala mkali miongoni mwa wasomi na wanasiasa nchini.

Wakizungumza na Mwananchi kwa nyakati tofauti jana kuhusu hali hiyo na taswira waionayo kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2020, wadau hao wamesema ulipaswa kufuatwa utaratibu kwa Membe kuitwa na si kutuhumiwa hadharani.

Hali hiyo imemfanya Profesa Mwesiga Baregu kwenda mbali zaidi na kubainisha kuwa hiyo ni nafasi nzuri kwa wapinzani katika uchaguzi mkuu huo ujao.

Sakata hilo lilianza baada ya Dk Bashiru akiwa mkoani Geita kumtaka Membe, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa afike ofisini kwake kujieleza.

Dk Bashiru alikuwa akijibu ujumbe uliotumwa kwenye akaunti ya mtandaoni ya mtu mwenye jina la Bernard Membe kujibu wito uliotolewa na Dk Bashiru akiwa Geita.

Dk Bashiru alimtuhumu Membe kuandaa mpango wa kumkwamisha John Magufuli katika uchaguzi wa urais na kwamba tangu ateuliwe hajawahi kuonana na mbunge huyo wa zamani za Mtama.

Membe alieleza kushangazwa na utaratibu uliotumika kumuita na akabainisha kuwa pengine ni ugeni kazini wa Bashiru, lakini akaahidi kwenda kumuona akirudi safari ya nje ya nchi.

Katika ujumbe huo wa twitter uliotumwa na mtu mwenye jina kama la Membe alisema atakapokwenda ofisini kwa Dk Bashiru, mtu anayemtuhumu kuandaa mkakati wa kumng’oa Rais Magufuli, naye awepo ili athibitishe tuhuma hizo.

Licha ya Dk Bashiru kurudia kutoa wito huo na kukataa masharti ya Membe aliyetaka aliyemtuhumu akathibitishe, jambo hilo halijapita bila maoni ya wadau.

Mwanasheria na wakili, Dk Onesmo Kyauke alisema, “Inaonekana (CCM) wana taarifa fulani kuhusu harakati za Membe ndio maana walitumia njia ile (ya Bashiru) kumuita. Kama ingekuwa kawaida si wangeweza kumuita (Membe) kimyakimya tu.

“Staili iliyotumika kumuita ni kama kutaka kutoa ujumbe kwa jamii. Binafsi sioni kama ni tatizo kwa uchaguzi ujao maana CCM wana utaratibu wao kuwa rais aliyepo madarakani hupitishwa tena kugombea kwa awamu ya pili.”

Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Uhusiano wa Umma wa Chama cha Wananchi (CUF), Abdul Kambaya alisema anashangaa kuitwa kwa Membe kwa sababu waliotajwa kwa tuhuma hizo wako wengi akiwamo Abdulrahman Kinana na Yusuph Makamba.

Kambaya alisema kuna tatizo katika kushughulikia suala hilo kwa sababu halikutakiwa kwenda kwa umma, badala yake alitakiwa kumwandikia barua ya kumwita. Alisema njia aliyoitumia Dk Bashiru si sahihi na inaibua maswali. “Wametajwa wengi kwenye list (orodha) lakini kwanini Membe? Katibu Mkuu aseme kwanini Membe na siyo Kinana, kwanini siyo Makamba,” alisema Kambaya na kubainisha kuwa chama hicho kitakuwa na mgogoro mkubwa wa ndani.

Katika maelezo yake Profesa Baregu ambaye ni mjumbe wa kamati kuu ya Chadema alisema, “Membe amejibu vizuri kidiplomasia. Ila naona huu ni mwanzo wa mwisho wa CCM ni kama kuna makundi sasa.”

“Mambo (kwa CCM) yanaweza kuwa magumu maana wanaweza kupata mgombea ila asiungwe mkono na wanachama wake wakachukua hatua.”

Alisema hiyo ni fursa kwa wapinzani maana wakiendelea kulumbana huenda ikafika wakati wakashindwa kuelewana kabisa.

Profesa Gaudence Mpangala wa Chuo Kikuu Katoliki cha Ruaha (Rucu), alisema chama kilitakiwa kufanya uchunguzi wake kwanza badala ya kukimbilia kumhoji mtuhumiwa.

“Kumhoji pekee siyo njia ya kupata majibu, atakwambia sihusiki baada ya hapo unafanyaje? Bashiru autafute ukweli kwanza na siyo kusubiri Membe aje kumthibitishia,” alisema Mpangala.

Akiwa na mtazamo kama huo, Mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Dk Stephen Kombe alisema atakachojibu Membe watakapokutana kiko wazi, hivyo hakukuwa na haja kwa Dk Bashiru kumwita.

Hata hivyo, alisema ukimya wa Membe umekuwa ukiwasumbua CCM kwa sababu hawajui anafikiria nini. Alisema; “mtu akiwa mzungumzaji sana, ni rahisi kujua fikra au hisia zake kuliko yule ambaye hazungumzi kitu.”

Mwenyekiti wa Chama cha Umma (Chaumma), Hashimu Rungwe alisema njia aliyotumia Dk Bashiri kumwita Membe haikuwa sahihi kwa sababu Membe ni mtu anayefahamika na ni rahisi kumpata.

“Katibu Mkuu kama anamheshimu Membe, angemwandikia barua rasmi ya kumwita, Membe alikuwa kiongozi mkubwa Serikalini, sijui yeye anamchukuliaje,” alisema Rungwe na kusema kumwita mwanachama wake si tatizo, lakini angemwita pia mtu aliyemtuhumu Membe.

Katibu Mkuu wa Chama cha Kijamii (CCK), Renatus Muabhi alisema Membe ni kiongozi mwenye ushawishi mkubwa na kwamba, ushawishi huo unaweza kuongezeka zaidi kwenye sakata hili kama Dk Bashiru ataendelea kumfuatilia.

“Membe ni mwanasiasa mzoefu, ana watu wengi nyuma yake. Kwa hiyo, unapomshushia tuhuma lazima uwe na ushahidi, ” alisema.

Hili suala linaongeza tension na kumuweka Membe kwenye ramani,” alisema Muabhi.