Membe atua nchini, afunguka

Dar es Salaam. Aliyekuwa kada wa CCM, Bernard Membe amerejea nchini jana akitokea nchini Afrika Kusini ambako alikuwa akimuuguza mwanaye, huku akifunguka zaidi kuhusu uamuzi wa kamati kuu ya chama hicho kumvua uanachama.

Membe aliyefukuzwa uanachama wake CCM wiki iliyopita kutokana na sababu za kinidhamu, alifika nchini saa 09:15 kwa ndege ya Shirika la Ndege la Kenya (KQ) namba 484.

Alipoulizwa sababu za kupitia Nairobi alisema alifanya hivyo kwani alikwenda kumjulia hali aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya, Raphael Tuju ambaye alipata ajali wakati wa mazishi ya Rais mstaafu, Daniel arap Moi.

Baada ya kutua nchini, Membe aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, aliwasiliana na Mwananchi kwa maandishi akituma ujumbe unaoikosoa Kamati Kuu ya CCM kutangaza uamuzi wa kumvua uanachama, kabla ya kuidhinishwa na Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC).

“Kamati Kuu ilifanya haraka (rushed judgment) kutangaza mapendekezo yake na kuufanya umma uamini kuwa hayakuwa mapendekezo, bali ni uamuzi kamili. Mchakato huu ulianzia NEC na ni vyema taratibu zikafutwa ili uishie NEC,” alisema Membe na kuongeza:

“Naomba tu niseme kwamba niliipata taarifa ya kufukuzwa kwangu kutoka CCM mpya tarehe 28/2/2020 kwa njia ya tangazo la (Humphrey, katibu wa Itikadi na Uenezi) Polepole kwa waandishi wa habari.

“Hadi leo, sijapokea barua ya kufukuzwa kwangu kwa sababu Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ambayo inatakiwa kupokea na kujadili mapendekezo ya Kamati ndogo ya maadili na nidhamu na ya Kamati Kuu bado haijakutana,” alifafanua.

Itakumbukwa kuwa baada ya tangazo la kuvuliwa uanachama na Kamati Kuu, Membe alisema hakuwa na kosa lolote na kwamba tatizo kubwa ni nia yake ya kugombea urais kupitia CCM akitaka kupambana na Rais John Magufuli.

“Tatizo ni urais. Wala wasipindishe pindishe mara oooh maadili..eti siju kafanya nini…..shida kubwa ni urasi,” alisema Membe alipozungumza na Mwananchi Februari 28 mara baada ya CCM kutangaza kumfukuza.

Baadaye Katibu Mkuu wa CCM, Bashiru Ally akizungumza na Wahariri wa Kampuni ya Mwananchi Communications Ltd (MCL) jijini Dar es Salaam alimtaka Membe ‘kutuliza akili’ kwani mchakato wa suala lake ulikuwa haujafikia mwisho.

“Mimi sijamuandikia barua mpaka sasa, nasubiri idhini ya NEC maana ndiyo walitutuma kuwaita wanachama hawa na sisi tumetekeleza. Sasa na yeye atulie maana hili ni jambo kubwa, hata lingenikuta ningehitaji ushauri wa marafiki zangu pengine na mke wangu,” alisema Dk Bashiru.

Jana Membe alisema mpaka hapo NEC itakapokutana na yeye kuandikiwa barua ya kufukuzwa, hatakuwa na cha kusema. “…nawaomba tuvute tubira na tuipe NEC haki yake ya kujadili na kuidhinisha adhabu hiyo,” alisema Membe na kuongeza:

“Nina hakika wajumbe wa NEC wataambiwa kuwa kwenye Kamati ya maadili tulikubaliana kuwa masuala au madai yote ya kisiasa na ya kiuchumi ambayo Musiba (Cyprian) alikuwa anayaporomosha dhidi yangu kila kukicha, yasijadiliwe kwa sababu yapo mahakamani.”

Alisema Kamati hiyo ilijadiliana naye jambo moja tu lililohusu taarifa ya udukuzi. “Katika udukuzi huo mimi nilidukuliwa nikiwa natoa maoni yangu kuhusu waraka ambao Mzee (Yusufu) Makamba na Mheshimiwa (Abdulrahman) Kinana waliuandika.”

“Baada ya hapo tulijadili masuala mengi kwa ufasaha mkubwa. Nasubiri majadiliano na barua ya NEC ili nijue nahukumiwa kwa taarifa ya udukuzi au kwa madai mengi ambayo Musiba alikuwa akiyatoa dhidi yangu na ambayo Mahakama imesema Musiba anayo kesi ya kujibu”.

Membe alisema haamini kama NEC itaidhinisha adhabu dhidi yake kwa masuala ambayo yako mahakamani kwani kufanya hivyo itakuwa ni kuikwaza mahakama.

“Kuna haraka gani kutoa adhabu kwa madai ambayo mimi nimemburuza mtu huyo mahakamani. Kama ni adhabu inayotokana na udukuzi, Katiba inasema nini kwenye ibara ya 18c?” alihoji.

“Ndiyo maana naomba tusubiri uamuzi wa NEC hata kama utalingana na mapendekezo ya Kamati Kuu. Nitauheshimu,” alisisitiza.