Meya Kinondoni aelezea jinsi Coco Beach itakavyoboreshwa

Muktasari:

Ufukwe wa Coco uliopo Dar es Salaam nchini Tanzania unatarajiwa kuanza kuboreshwa kuanzia Septemba mwaka 2019 ili kuuweka katika mandhari nzuri.

Dar es Salaam. Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Dar es Salaam nchini Tanzania, Benjamini Sitta amesema maboresho ya ufukwe wa Coco yataanza rasmi Septemba, 2019.

Sitta alitoa kauli hiyo jana Alhamisi Agosti 15,2019 wakati wa mazungumzo na waandishi wa habari ikiwa zimepita siku sita tangu Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kufanya ziara katika ufukwe huo na kutoa mwezi mmoja kwa uongozi wa Halmashauri ya Kinondoni kukamilisha mchakato huo aliodai unachelewa kwa sababu ya uzembe.

Hata hivyo, Meya Sitta alisema kuchelewa kwa maboresho hayo kumetokana na sheria na taratibu za manunuzi.

“Fedha ipo anayesubiriwa sasa ni mkandarasi ambaye atakidhi vigezo hakuna makandokando yoyote wala upigaji fedha na tunamuhakikishia kiongozi wetu mkuu wa mkoa kuwa tutakamilisha kama alivyoagiza,” alisema.

Alisema katika ufukwe huo yatatengwa maeneo mbalimbali kwa ajili ya kupumzika watu, uwanja wa mpira na sehemu za michezo mbalimbali pia hakutakuwa na majengo ya moja kwa moja.

“Pia majengo yake yatakuwa tofauti na majengo mengine, hatutajenga ya moja kwa moja bali yale ambayo yanaweza kuhamishika ili mandhari ya fukwe yasiharibike, lakini pia tutaboresha mazingira mazuri kwa wafanyabiashara wakiwemo wauza mihogo,” alisema Sitta.

Maboresho hayo yatakayo gharimu Sh14 bilioni yanatarajiwa kumalizika ndani ya miezi sita na yanalenga kutoa fursa mbalimbali za kitalii kwa wananchi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa mipango miji, ujenzi na mazingira wa manispaa hiyo, Songoro Mnyonge alisema mchakato na maandalizi ya mradi huu yanaendelea vizuri na yatamalizika ndani ya muda uliopangwa.

Aidha ameomba baadhi ya watumishi kuacha mara moja kupeleka taarifa kwa viongozi ambazo si sahihi ili kuepusha mkanganyiko wa taarifa za miradi.

‘Sisi tumepokea maagizo hayo, tunajua wapo watu wachache ambao wanania ya kutuchonganisha na kiongozi wetu hata hivyo hizi kwetu tumezichukua kama changamoto ambazo sasa zitatufanya sisi tufanye kazi hii kwa manufaa ya wananchi wa Kinondoni na taifa kwa ujumla,” alisema Mwenyekiti huyo.