Mkandarasi awekwa ndani kwa kushindwa kutekeleza mradi kwa wakati

Mkuu wa wilaya ya Tanganyika Salehe Mhando akitoa onyo kwa Kaimu Meneja Tarura Maila Richard kuhusu kushindwa kuchukua hatua juu ya mkandarasi wa Kampuni LGNA kutokana na kusua sua mradi wa ujenzi barabara ya Mkokwa- Mnyagala. Picha na Mary Clemence.

Katavi. Mkandarasi wa kampuni ya LGNA  aliyekuwa akijenga barabara ya Mkokwa-Mnyagala halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika mkoani Katavi amefukuzwa kazi kwa kushindwa kutekeleza mradi kwa wakati.

Mbali na kufukuzwa anashikiliwa  na Takukuru kwa agizo la mkuu wa Wilaya ya Tanganyika,  Saleh Mhando.

Katika ziara yake ya kushtukiza Machi  19, 2020  alichukua hatua hiyo na kuwapa onyo Mamlaka ya Barabara mijini na vijijini (Tarura) na kuwatahadharisha mameneja wa Tarura kuhusu mkandarasi huyo kutofanya kazi vyema  lakini hakuna hatua iliyochukuliwa dhidi yake.

"Nimekutahadharisha mara nyingi ili ujiongeze, najua  ulikomtoa wanalia ni mkandarasi feki, namfukuza kazi kuanzia sasa abebe mizigo yake. Kamanda wa Takukuru mchukue huyu uwafanyie uchunguzi na hawa Tarura ili ubaini kama alikuwa na sifa, na wewe kaimu meneja ndani ya siku tatu apatikane  mwingine aanze ujenzi."

"Fedha zipo tangu mwaka 2019, umesaini mkataba Oktoba 2019, mpaka sasa hakuna ulichokifanya tofauti na kumwaga kifusi  mradi unatakiwa ukamilike  April 9,2020 zimebaki siku ngapi? Tumeshindwa kupitisha vifaa kwenda kujenga kituo cha afya,  wananchi wanaendelea kupata shida wakati rais anatoa fedha ili kuboresha huduma katika jamii.

Mkurugenzi wa kampuni ya LGNA,  Michael Kessi baada ya kuhojiwa kuhusu kuchelewa kukamilisha mradi huo amesema ameshindwa kutekeleza kwa wakati kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha.

" Tulishauriana na wataalamu kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha maji ni mengi tukakubaliana nisitishe, nianze kujenga  makaravati hadi hali itakapokuwa nzuri," amesema Kessi.

Kwa upande wake kaimu meneja Tarura wilaya ya Tanganyika,  Maila Richard amesema licha ya kutoa maelekezo kwa mkandarasi huyo anakaidi na  kuendelea  kujenga kinyume na utaratibu unaotakiwa.

"Kazi ameifanya kinyume na utaratibu tulivyohitaji sisi kimkataba  have grade siyo sahihi, anatakiwa ainue tuta baada ya hapo amwage kifusi lakini hafanyi hivyo, wiki iliyopita nilimpa maelekezo. Jumatatu akaendelea tena, nimemwandikia barua kifusi hiki akitoe afuate utaratibu unaotakiwa ili wananchi waweze kupita na yeye aendelee na kazi zake,

 

 

Baadhi ya wananchi,  Joseph Emmanuel na Charles Ng'wandu  wamesema hali hiyo inawaathiri kiuchumi kutokana na magari kukwama mara kwa mara, waendesha pikipiki na baiskeli nao  wanapata usumbufu.

" Nimebeba tani 10 za mchele kupeleka Bariadi lakini gari limekwama tangu juzi, tunaomba serikali ichukue hatua barabara imewekewa kifusi muda mrefu lakini hakuna kinachoendelea,  tunaotumia baiskeli kubeba mizigi tunasumbuka  sana kupita," wamesema

Barabara hiyo yenye urefu wa kilometa 1.5 inatakiwa kujengwa kwa Sh74 milioni ambapo imefikisha wakandarasi watatu wanaofukuzwa bila kupata malipo  kwa kushindwa kutekeleza mradi  kwa wakati.