Mke wa Kusaga na Diamond wamiliki Wasafi Televisheni

Muktasari:

Kituo hicho kipya cha televisheni kimezua mjadala kuhusu wamiliki wake tangu kilipoanza matangazo ya majaribio, baadhi wakisema kinamilikiwa kwa asilimia 100 na nyota huyo wa Bongo Fleva.

Dar es Salaam. Swali kuhusu nani ni mmiliki wa kituo kipya cha televisheni cha Wasafi TV limepata jibu; ni watu watatu, akiwemo Diamond Platinamuz.

Hayo yamejulikana baada ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kutoa tangazo lenye orodha ya wamiliki hao, likitaka maoni ya umma kabla ya kutoa leseni ya kuruhusu kituo hicho kianze matangazo.

Umiliki wa kituo hicho umekuwa ukizua mijadala tangu mwanamuziki huyo nyota wa miondoko ya Bongo Fleva aanze kukitangaza, akitumia kaulimbiu ya “ukombozi wa wasanii”.

Baadhi wamekuwa wakidai kuwa mmiliki ni Diamond na wengine wanasema Joseph Kusaga, mmoja wa manguli katika biashara ya burudani na ofisa mtendaji mkuu wa Clouds Media. Wanadai DJ huyo wa zamani anamtumia mwanamuziki huyo kutangaza televisheni hiyo.

Wakati mjadala huo ukiendelea, TCRA imetoa tangazo linalodokeza majibu ya mjadala huo.

Katika tangazo lake kwa umma, mamlaka hiyo imewataja wamiliki watatu wa televisheni hiyo, ambayo tayari ipo hewani.

TCRA imemtaja mtu anayeitwa Juhayna Zaghalulu Ajmy kuwa anamiliki asilimia 53, wakati Nassibu Abdul Juma, ambaye ni Diamond, anamiliki asilimia 45 na Ali Khatib Dai anayemiliki asilimia mbili.

Juhayna ni mke wa Kusaga na amekuwa akionekana naye hadharani katika hafla tofauti za Clouds FM na nyingine.

“Kwa mujibu wa Kifungu cha 8 cha Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta, Sura ya 306 ya Sheria za Tanzania, maoni ya maandishi yanakaribishwa kutoka kwa mtu anayeguswa kuhusu kutolewa leseni kwa mwombaji na yaifikie Mamlaka ndani ya siku 14 tangu kuchapishwa kwa tangazo hili,” linasema tangazo hilo la mwezi Novemba.

“Maoni hayo yatazingatiwa wakati Mamlaka itakapokuwa ikifikiria kutoa leseni.”

Kampuni ya Wasafi, ambayo pia inamiliki lebo ya muziki ya Wasafi, inaonekana kutaka kuingia kwenye ushindani na Clouds Media, ambayo inamiliki kituo cha televisheni cha Clouds TV na redio ya Clouds FM.

Clouds Media hujishughulisha zaidi na biashara ya burudani, ikiwa na kampuni ndogo zinazosimamia wanamuziki na studio za kurekodi muziki, hali kadhalika kuandaa matamasha ya muziki.

Wamiliki wa Clouds pia wana kampuni zao tofauti zinazofanya kazi pamoja na Clouds media kama Primetime Promotions, Tanzania House of Talents, Choice FM na nyingine za michezo ya bahati nasibu.

Hata hivyo, wengi wamekuwa wakichukulia ushindani huo kuwa ni kiini macho kutokana na kuhisi kuwa Kusaga, ambaye ni ofisa mtendaji mkuu wa Clouds Media, ana hisa katika televisheni ya Wasafi TV, hivyo ndugu wawili hawawezi kugombana.

Mzozo wa pande hizo mbili umesababisha nyimbo za Diamond kutochezwa na vituo vya Clouds.

Mwishoni mwa wiki iliyopita, kampuni hizo mbili zilipambana katika sakata la uandaaji wa matamasha. Ingawa matamasha hayo mawili--Wasafi Concert lililofanyika Mtwara, na Fiesta Festival lililopangwa kufanyika Dar es Salaam yalikuwa mikoa miwili tofauti.

Baada ya Fiesta kuzuiwa, Diamond alituma video fupi Instagram akinywa soda na baadaye kutoa kicheko kirefu, mithili ya mtu anayemcheka mshindani wake kwa kutofanikiwa.