VIDEO: Mo Dewji aibua mjadala mtandaoni, aomba radhi

Muktasari:

  • Ujumbe ambao Mfanyabiashara maarufu nchini Tanzania, Mohamed Dewji ‘Mo’ ameuweka katika akaunti yake ya Twitter umezua mjadala ikiwamo wachangiaji kukumbushia kutekwa kwake na watu wasiojulikana alfajiri ya Oktoba 11, 2019 jijini Dar es Salaam.

Dar es Salaam. Mfanyabiashara maarufu nchini Tanzania, Mohamed Dewji ‘Mo’ ameibua mjadala mtandaoni baada ya kuweka ujumbe uliowaibua wachangiaji kumbushia tukio la kutekwa kwake.

Mo ambaye ni mwekezaji wa Klabu ya Simba jana Jumanne Septemba 17, 2019 aliweka ujumbe kwenye akaunti yake ya Twitter akisema, “Kuna maisha ya mtandaoni na maisha halisi.”

Ujumbe huo umejadiliwa kwa mitizamo tofauti huku wengine wakikumbushia bilionea huyo namba moja kijana Barani Afrika alivyotekwa na watu wasiojulikana jinsi watu walivyotumia mitandao hiyo kupaza sauti zao.

Alfajiri ya Oktoba 11 mwaka 2018, Mo alitekwa na watu wasiojulikana maeneo ya hoteli ya Collessium jijini Dar es Salaam alikokwenda kwa ajili ya mazoezi.

Tukio la kutekwa kwake lilitikisa ndani na nje ya nchi na mitandao mbalimbali ilijadili suala hilo la kutekwa kwake hadi Oktoba 20, 2019 watekaji walipomtelekeza akiwa hai katika viwanja vya Gymkhana Dar es Salaam.

Mwanaharakati Maria Sarungi akichangia ujumbe wa Mo ameweka picha ya mtoto ameshika shavu na kuandika, “#BringBackMo ilikuwa maisha ya mtandao au maisha halisi?#TutaelewanaTu.”

Baada ya Sarungi kuandika hivyo pamoja na wachangiaji wengine, Mo amemjibu akisema, “Nisamehe sana dada yangu (Sarungi). Naona umeichukulia tweet yangu out of context. Narudia kuwashukuru wote ambao mliniombea na kunisemea.”

Kisha Maria Sarungi akajibu, “Pole sana kaka, unajua kuna kijana msanii alikuja hapa kusema eti hizi kampeni za #BringBack ni za kufikirika na za mitandaoni ila kiuhalisia hakuna utekaji...sasa tushakuwa sensitive mtu akibeza “mambo ya mitandaoni” ndo maana niko hivi.Haya tuchanje mbuga.”

Msanii wa muziki nchini Tanzania, Lady Jay Dee akichangia ujumbe huo amesema, “Nadhani (Mo) alimaanisha watu wanaoishi maisha ya uongo kuonyesha vitu ambavyo hawana katika maisha yao halisi.”

“Hasa watu wengi maarufu wana hizo sana. Hata kupigia picha juice ambayo sio yako na kui post nayo ni maisha ya mtandaoni,” amesema Jay Dee

Thabitimketo amesema, “Maisha ya mtandaoni yakoje mkuu.” Huku Ndyanabo akihoji, “lipi unalipa nafasi kubwa kati ya hayo mawili!? na ya mtandaoni ni yapi na halisi ni yapi?  tujue mapema yawezekana waliopiga kelele humu ili uachiwe walikuwa wanajichosha bure na kujipendekeza.”