Moi kuanza upasuaji wa ubongo Machi 2020

Thursday February 20 2020

 

By Emmanuel Mtengwa, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Taasisi ya Tiba ya Mifupa (Moi) itaanza kufanya upasuaji wa ubongo bila kufumua fuvu la kichwa mwezi Machi, 2020 baada ya kukamilisha ujenzi wa maabara ya kisasa ya upasuaji wa ubongo katika taasisi hiyo.

Hayo yamebainishwa leo Alhamisi Februari 20, 2020 na mkurugenzi mtendaji wa taasisi hiyo, Dk Respicious Boniface katika ufunguzi wa maadhimisho ya siku ya madaktari yanayofanyika katika ukumbi wa kimataifa wa mikutano wa Mwalimu Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam.

Dk Respicious amesema hatua hiyo inatokana na Serikali kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa maabara ya kisasa inayotarajiwa kukamilika mwezi ujao.

“Ujenzi wa maabara ya kupasua ubongo, hii kitu ilikuwa haipo na hatukuwahi kutegemea kuwa itakuwepo, mwaka jana Rais (John Magufuli) ulitoa Sh7.9 bilioni kwa ajili ya ununuzi na usimikaji wa mashine hiyo.”

“Tunavyoongea sasa hivi, mashine zishafika pale Moi na makandarasi wanamalizia chumba kwa ajili ya kuisimika itakuwa tayari kutumika tarehe Machi 15,” amesema.

Amesema uwepo wa maabara hiyo utaifanya Tanzania kuwa moja ya nchi chache Afrika zinazotoa huduma hiyo.

Advertisement

“Mashine hiyo itawezesha taasisi ya Moi kufanya upasuaji wa ubongo kwa watu wenye matatizo ya mishipa ya damu kichwani pasipo kulazimika kufunua fuvu la kichwa” amesema

Mapema akitoa taarifa ya rasilimali watu na weledi wa kitaaluma, Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Profesa Lawrence Mseru amesema nchi inakabiliwa na upungufu mkubwa wa madaktari bingwa licha ya uhitaji wa wataalamu hao kuwa mkubwa.

Profesa Mseru ambaye pia ni mlezi wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT) amebainisha eneo ambalo ni changamoto zaidi kwenye madaktari bingwa akisema kuna uhaba mkubwa wa wataalamu wa kutoa dawa za usingizi.

“Kuna upungufu wa madaktari bingwa na ubingwa bobezi katika fani zote kwa mfano katika fani nyingine kama wataalum wa kutoa dawa za usingizi, upungufu ni mkubwa sana jambo ambalo linaweza kuathiri utoaji wa huduma ya upasuaji salama,” amesema Profesa Mseru.

Mkutano huo unaoendelea umehudhuriwa na Rais John Magufuli; naibu Waziri wa Afya, Dk Faustine Ndugulile; Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwangalla na viongozi mbalimbali wa Serikali.

Advertisement