Moto mlima Kilimanjaro wadhibitiwa kwa asilimia 98

Askari wa Wanyamapori wakiwa katika mlima kilimanjaro kuangalia sehemu ambayo maafa ya moto hayajafika. Nampiga picha maalum

Muktasari:

Moto uliozuka katika Hifadhi ya Mlima Kilimanjaro nchini Tanzania Oktoba 11, 2020 umedhibitiwa kwa  asilimia 98  hadi kufikia leo asubuhi Oktoba 17, 2020.

 

Moshi. Moto uliozuka katika Hifadhi ya Mlima Kilimanjaro nchini Tanzania Oktoba 11, 2020 umedhibitiwa kwa  asilimia 98  hadi kufikia leo asubuhi Oktoba 17, 2020.

Moto huo ambao umeteketeza Kilomita za mraba 95.5 sawa na asilimia tano ya eneo lote la hifadhi hiyo la kilomita za mraba 1,700, ulianzia eneo la Whona ambako ni kituo cha kupumzikia wageni wanaotumia njia ya Mandara na Horombo.

Hayo yameelezwa leo na kamishna mwandamizi wa uhifadhi Tanapa Kanda ya Kaskazini, Herman Batiho wakati akipokea msaada wa katoni 300 za maji kutoka Shirika lisilo la kiserikali la Kijani Pamoja.

"Mpaka asubuhi ya leo moto umedhibitiwa kwa asilimia 98, yapo maeneo machache ambayo yalionekana na moto na tayari vikosi vya askari vipo maeneo mbalimbali ya hifadhi hii vikiendelea kudhibiti moto huo na wengine wakizunguka kwa ajili ya kufuatilia na kuchukua tahadhari.”

“Msaada huu wa maji utatusaidia kwani bado kuna kazi inaendelea ya uzimaji na ufuatiliaji lakini pia niombe wadau wengine wajitokeze kutoa msaada ili kukabiliana na janga hili kwani mlima huu una faida nyingi kiuchumi"

Mwenyekiti wa Shirika hilo, Fredrick Marealle amesema wametoa msaada huo kama njia ya kuunga mkono juhudi za serikali za kudhibiti moto huo.

Shirika la Kijani Pamoja linatekeleza mradi wa Kilimanjaro ambao unalenga kutunza mazingira kwa kupanda miti na kutoa elimu juu ya utunzaji wa mazingira nchini.

Shughuli za utalii katika Hifadhi ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro, zinaendelea kama kawaida na hazijaathiriwa na moto huo.