Msabaha: Wanaonikosoa kuichangia UVCCM hawajui siasa za Z’bar

Dar es Salaam. Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Maryam Msabaha amedai wanaomkosoa na kumshutumu kwa kitendo cha kuwachangia Sh500,000 vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) hawazijui siasa za Zanzibar.

Jumamosi iliyopita, katika shughuli ya kuweka jiwe la msingi la Shule ya Mwanakwerekwe huko Unguja, Rais John Magufuli alipitisha harambee ya kuwachangia vijana wa UVCCM waliotumbuiza kwa nyimbo.

Miongoni mwa waliochangia alikuwa Rais Magufuli aliyetoa Sh2 mlioni huku Msabaha akichangia Sh500,000 hali iliyoibua mjadala hasa miongoni mwa wanachama wa chama chake.

Tofauti na wachangiaji wengine waliokuwa wanatamka kiasi watakachochangia na kurudi kukaa kwenye eneo lao, hali ilikuwa tofauti kwa Msabaha ambaye baada ya kutoa ahadi yake, aliitwa jukwaa kuu na Rais Magufuli.

“Huyu ni mbunge wa Chadema na amechangia hawa vijana wa CCM,” alisema Rais Magufuli huku umati uliojitokeza ukishangilia.

Hata hivyo, hatua hiyo imezua mjadala kwani baadhi ya wanachama wa chama chake wamehoji sababu ya yeye kutoa fedha hizo kwa chama washindani wake lakini asitoe kwa chama chake.

Msabaha aliiambia Mwananchi jana kuwa alifanya vile kwa kuwa lile ni eneo lake la kisiasa.

“Mkoa wa Mjini Magharibi ni eneo langu la kisiasa na wale vijana ni wale wanaotafuta ajira, wako makambini na mimi kama mama na mwanasiasa ninayepigiwa kura na wana CCM, sioni tatizo,” alisema Msabaha.

Mbunge huyo aliyeanza siasa za upinzani mwaka 1992 akiwa NCCR-Mageuzi kisha kuhamia TLP na sasa yupo Chadema alisema, “ukiwa mwanasiasa hupaswi kuwa na chuki, tunapaswa kuwaonyesha wenzetu kuwa siku tukichukua nchi hatutakuwa na chuki.”

“Lakini pale pia nilikitangaza chama changu na isitoshe nilikaa VIP (jukwaa la wageni mashuhuri) sasa wote wananyanyuka kwenda kuchangia mimi nibaki nimekaa? Mbona Rais akiwa kwenye ziara majimbo ya bara, wabunge wa Chadema wanakwenda, tatizo wanaonikosoa hawaijui siasa za Zanzibar, ” aliongeza.

Aliwaasa wabunge wenzake na wanachama wake kwa kuwaeleza kama kuna mtu hawampendi wanapaswa kutomwonyesha chuki.