Msigwa: Chadema haina fedha ya kununua watu

Monday December 02 2019
pic msigwa

Dar es Salaam. Mshtakiwa wa pili katika kesi inayowakabili viongozi tisa wa Chadema, Mchungaji Peter Msigwa amesema Waziri Mkuu mstaafu, Fredrick Sumaye hakununuliwa bali alihamia chama hicho kwakuwa anakipenda.

Msigwa ambaye pia ni Mbunge wa Iringa Mjini, ameeleza hayo leo Desemba 2, 2019 wakati  akihojiwa na Wakili Mkuu wa Serikali, Jackline Nyantori baada ya kuulizwa kuwa walimnunua kwa shilingi ngapi.

Msigwa alidai chama hicho hakina fedha ya kununua watu, hivyo Sumaye alihamia chama hicho kwa kuwa anakipenda.

“Waitara alinunuliwa kwa kuahidiwa Uwaziri mimi sikushiriki, lakini niliona mazingira,” alisema Mchungaji Msigwa.

Akiendelea na utetezi mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba, Msigwa alidai katika mkutano wa kufunga kampeni za uchaguzi mdogo wa marudio Jimbo la Kinondoni,  Februari 16, 2018 wapo wabunge waliokuwepo ambao hawapo Mahakamani.

Alidai Wabunge hao ni aliyekuwa Mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara, Mbunge wa Tunduma, Frank Mwakajoka, Mbunge wa Ubungo, Saidi Kubenea, Mbunge  wa Ndanda Cecil Mwambe na Mbunge wa Kilombero, Peter Lijualikali.

Advertisement

Alipoulizwa alipataje taarifa ya kuhudhuria kwenye mkutano huo wa kufunga kampeni wakati yeye ni Mbunge wa Iringa, Msigwa alidai alipewa taarifa kupitia kwenye sekretarieti ambayo inaongozwa na Katibu Mkuu Dk Vicent Mashinji.

“Tuliitwa wabunge mbaalimbali kuhamasisha ili kuleta mabadiliko tunayoyapigania katika nchi hii,” alidai Msigwa

Aidha, Msigwa alidai kuwa kama mjumbe wa kamati kuu alishiriki kumteua mgombea ubunge, Salum Mwalimu ili kukiwakilisha chama hicho katika uchaguzi wa marudio.

Akiendelea kuhojiwa, Msigwa alidai kuwa maelezo ya Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, (IGP) na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Akwiline aliuwawa eneo Ia Kinondoni.

Akihojiwa na Mkurugenzi Msaidizi wa Mashtaka Joseph Pande kama kutembea na Silaha ni kosa Msigwa alidai kutembea na silaha sio kosa kwani inategemea ni kwenye muktadha gani.

“Mtu yuko huru kutembea na silaha yake popote na ahitaji kibali cha polisi, alidai Msigwa.

Alidai siku ya kampeni hakuhamasisha hadha bali aliongea na hadha ya wanachi waliokuwepo kwenye mkutano.

Mbali ya Msigwa, washtakiwa wengine  ni Mwenyekiti wa Chama hicho Freeman Mbowe,Katibu Mkuu, Dk Vicent Mashinji, Manaibu katibu wakuu, John Mnyika (Bara) na Salum Mwalimu (Zanzibar) na mbunge Tarime John Heche.

Wengine ni Mbunge wa Peter Msigwa na Mwenyekiti wa Kanda ya Serengeti , Esther Matiko na Mwenyekiti wa Baraza Wanawake (Bawacha), Halima Mdee, na mbunge wa Bunda Ester Bulaya

Mbowe na wenzake wanakabiliwa na Mashtaka 12 likiwamo la uchochezi, kufanya mkusanyiko usio halali na kukaidi amri ya jeshi la polisi.

Advertisement