Msomi wa cheti aliyepambana hadi kuunasa ukurugenzi TMA

Usemi wa wanawake wakiwezeshwa wanaweza ni maarufu hasa kwa wanawake lakini wapo wanaopingana na usemi huo kwa vitendo wakisimama na kujiwezesha wenyewe hadi kufikia malengo yao.

“Sikusoma moja kwa moja hadi kufika hapa nilipo, nilianza na cheti na sasa ni daktari (PhD), nilichokuwa natamani ni kusoma masomo ya sayansi, nilifanikiwa hadi leo ninaogelea huko,” ndivyo Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania, (TMA) Dk Agness Kijazi anavyoanza kuelekezea safari ya maisha yake.

Julai 27, 2018 Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) Antonio Guterres alimteua Dk Kijazi kuwa mjumbe wa kamati ya Umoja wa Mataifa ya watu 10 itakayotoa msaada na ushauri wa masuala ya teknolojia (TFM) kwa Umoja huo.

Uteuzi huo ulifanyika kufuatia uamuzi wa nchi wanachama wa UN kuhitaji kuwa na wajumbe 10 wa kuushauri umoja huo katika masuala ya sayansi, teknolojia na ubunifu katika mchakato wa kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu yaani SDGs.

Mchakato wa uteuzi huo ulizingatia sifa mbalimbali ukiwemo ubobezi wa taaluma na heshima kwa nchi zao ili waweze kutumikia kamati hiyo kwa miaka miwili.

Kupitia nafasi hiyo amekuwa mwakilishi wa kudumu wa Tanzania katika Shirika la Utabiri wa Hali ya Hewa Duniani (WMO).

Pia ni mwanamke wa kwanza kutoka Afrika Mashariki na wa pili Afrika kuchaguliwa kuwa mjumbe wa Baraza Kuu la WMO sambamba na kushika nyadhifa nyingine za juu kwenye kamati za shirika hilo kikanda na kimataifa.

Dk Kijazi ana shahada ya uzamivu (PhD) katika masuala ya hali ya hewa aliyoipata Chuo Kikuu cha Cape Town nchini Afrika Kusini.

Haikuwa rahisi kufika alipo

Dk Kijazi anasema kama mwanamke haikuwa rahisi kufika kote huko. “Changamoto ya kwanza niliyokutana nayo baada ya kumaliza masomo ya diploma ya masuala ya hali ya hewa nilifunga ndoa.

“Kwa kuwa nilikuwa kuna mahali natamani kufika ilikuwa lazima nijiendeleze kielimu, huu ulikuwa mtihani wangu wa kwanza mgumu, namna gani nitamshawishi mume wangu kuhusu hilo hadi anielewe, ”anasema Dk Kijazi.

Anafafanua kuwa dhamira ya kufika mbali ilimpa ujasiri wa kuomba ridhaa hiyo kwa mumewe.

“Nilipata mtihani mwingine ambao kwa msaada wa mume wangu nilifaulu, aliniambia kama ninataka kujiendeleza kielimu nihakikishe na familia inaendelea.

“Nilichagua yote, nilipokwenda kuchukua shahada ya masuala ya hali ya hewa Chuo Kikuu cha Nairobi, Kenya nilijifungua mtoto wa kwanza,” anasema na kuongeza kuwa mumewe aliona tabu anayoipata, kusoma huku analea akamchukua mtoto akiwa na miezi sita. “Nilionyesha nia na dhamira ya kweli na mume wangu aliiona na kuendelea kuniunga mkono, alimchukua mtoto na kumnywesha maziwa na kumhudumia hadi nilipomaliza masomo,” anasema.

Anasema awali akiwa msichana alitamani kuwa daktari wa binadamu na ndiyo maana aliweka bidii kwenye masomo ya sayansi na baada ya kumaliza sekondari alijaribu kuchukua masomo ya hali ya hewa ngazi ya cheti. “Nikiwa huko nikabaini ni sayansi halisi kama ile niliyotamani kuisomea, nikaamua kubobea huko,” anasema.

Kazi na familia

Muda wa kazi na familia anasema nayo pia ni changamoto ingawa anajitahidi kujigawa na kila kimoja kukipa nafasi yake.

Anatumia muda mwingi kwenye kazi kuliko nyumbani, ingawa akipata nafasi hujitahidi kufanya shughuli za familia. “Asubuhi siondoki nyumbani kabla sijajua familia yangu itashindaje mchana na kuhakikisha kila kitu kipo sawa. Lakini nikipata nafasi napika na nipo vizuri sana kwenye kutayarisha vitafunwa, nalima bustani ya mboga mboga na maua na kuweka mazingira ya nyumbani vizuri,” anasema Dk Kijazi mama wa watoto watatu, kati yao wawili wakiwa pacha.

Watoto wake wote wamechagua sayansi, wa kwanza anachukua udaktari yupo chuo mwaka wa nne, wa pili mhandisi na wa tatu kafuata nyayo zake anasomea masuala ya hali ya hewa.

Dk Kijazi anaeleza siri ya kuwa mwanamke wa kwanza kushika nafasi ya umakamu wa tatu wa Rais wa WMO, kuwa ni kumcha Mungu, kujiamini na uchapakazi.

“Sikukubali kubaki nyuma, nilikuwa na nimekuwa na ari na nia ya kuitumikia na kuisaidia nchi yangu hususan katika huduma za hali ya hewa kwa jamii,” anasema.

Anasema amekuwa mjumbe wa kamati kuu ya WMO (WMO-Excutive Council) kwa miaka tisa na kwenye kamati ya watu 10 wanaomshauri Katibu Mkuu wa UN katika masuala ya ubunifu, sayansi na teknolojia. “Hii ni kukuonyesha jinsi gani nilivyopambana kufikia hapa, sikuridhika na pale nilipokuwa,” anasema.

Mafanikio ya TMA chini yake

Kuhusu mafanikio ya TMA chini ya uongozi wake anasema baadhi ni kupata cheti cha ubora wa kimataifa cha utoaji huduma za hali ya hewa katika sekta ya usafiri wa anga tangu mwaka 2011 (ISO 9001 :2008) na kuifanya Tanzania kuwa nchi ya kwanza kupata cheti hicho katika nchi za Afrika zilizo Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Mengine ni kupata ISO 9001: 2015 iliyopatikana mwaka 2017 na kuifanya Tanzania kuwa nchi ya tatu katika Afrika kuthibitishwa kabla ya Septemba 2018 ambayo ilikuwa ni tarehe ya mwisho ya matumizi ya cheti cha zamani.

Anasema pia amefanikiwa kupitia mabadiliko ambapo TMA imetoka kuwa wakala hadi Mamlaka kupitia sheria ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Na. 2 ya mwaka 2019 “Tanzania Meteorological Authority Act No. 2 of 2019.

“Sasa viwango vya usahihi wa utabiri wa hali ya hewa vimeongezeka kutoka asilimia 75 hadi kufikia kati ya 87 na 96.

“Mpaka sasa Mamlaka ya Hali ya Hewa ina rada mbili na mkataba wa kujenga na kusimika rada tatu ushasainiwa, lengo ni kuwa nazo saba,” anasema.

Anasema pia wamefanikiwa kusomesha wataalamu wa sayansi ya hali ya hewa ngazi ya shahada (BSc. Meteorology) nchini katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), awali wataalam hao walikuwa wakisomeshwa nje ya nchi kwa gharama kubwa. Kuhusu wanawake kukwama mahali anasema anayewakwamisha ni wao wenyewe kutokana na kuliangalia jambo kwenye changamoto zaidi ya kuzishinda.

Anafafanua hata yeye asingefikia hapo alipo kama angeogopa changamoto za awali.

“Wakati nimeolewa na nataka kujiendeleza kielimu, wapo marafiki zangu waliniambia Agness huwezi wakinitajia changamoto na ugumu nitakaokutana nao, kwa kweli walinieleza kitu halisi na kilichotokea.

“Mimi sikuwa pamoja nao, lengo langu halikuwa kuangalia changamoto, lilikuwa kufikia ninapokwenda bila kujali nitapita wapi, ndiyo maana nilisonga, wanawake wote wanaweza waishinde roho ya kukataa, kukatishwa tamaa.