Mtandao dawa za kulevya wazikabili nchi za Mashariki mwa Afrika

Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini(IGP) Saimon Sirro

Muktasari:

  • Usafirishaji haramu wa binadamu na dawa za kulevya bado changamoto  Mashariki mwa Afrika

Arusha. Nchi za Mashariki mwa Afrika bado zinakabiliwa na tishio la mtandao wa biashara  ya dawa za kulevya, usafirishaji binadamu, silaha za moto na baridi kutoka kwenye maeneo yasiyo na utulivu.

Akifungua kikao cha kamati tendaji na wakurugenzi wa makosa ya jinai kutoka nchi wanachama wa Shirikisho la Wakuu wa Polisi Mashariki mwa Afrika (EAPCCO), mkuu wa Jeshi la Polisi nchini(IGP) Saimon Sirro  amesema jitihada za pamoja zinahitajika kukomesha uhalifu.

Amesema matukio kigaidi yanayotokea maeneo mbalimbali duniani ni kiashiria kwamba nchi za ukanda wa Mashariki mwa Afrika  haziko salama.

Amesema ni vyema  kuboresha ushirikiano na kufanya vikao vya ujirani mwema baina ya nchi zetu kwa lengo la kuimarisha usalama, amani na utulivu ndani na nje ya mipaka kwa kuimarisha ushirikiano miongoni mwetu.

Awali, Kamishna wa Polisi na Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI) Robert Boaz akizungumza kwenye mkutano huo amesema mkutano huo unashirikisha wajumbe ambao ni wakurugenzi wa upelelezi wa makosa ya jinai.

Wengine ni wajumbe wa kamati ndogo za sheria, mafunzo, jinsia, uzuiaji wa makosa ya kigaidi wanaotoka nchi za Burundi, Comoros, Djobouti, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Eritrea, Ethiopia, Kenya, Rwanda Seychelles Somalia, Sudani Sudani Kusini, Uganda na Tanzania.

Amesema kikao hicho kinaongozwa na kauli mbiu ya Kuimarisha Ushirikiano na Ubunifu katika mapambano dhidi ya uhalifu unaovuka mipaka ndani nan je ya Mashariki mwa Afrika.

Mkutano wa mwaka wa 21 unaowakutanisha wakuu wa polisi wa nchi za Mashariki mwa Afrika unatarajiwa kufunguliwa Septemba 19, mwaka hu una Rais wa Tanzania John Magufuli mjini Arusha.