Mtume Mwingira aeleza sababu baba yake kuzikwa baada ya siku 30

Kibaha. Kiongozi wa Kanisa la Efatha, Mtume na Nabii Josephat Mwingira amesema alipata maono kutoka kwa Mungu kwamba mazishi ya baba yake Elias Mwingira aliyefariki dunia Januari 22, mwaka huu yafanyike jana Jumamosi februari 22.

Mwingira alieleza hayo jana katika ibada ya mazishi iliyofanyika Kibaha mkoani Pwani katika ukumbi wa kanisa hilo unaotumika kufanya makongamano uliopo katika eneo la kanisa lenye ukubwa wa takribani ekari 500.

“Baada ya msiba nilipata maono ya kuzika tarehe ya leo (jana) nilimshirikisha mke wangu na ndugu zangu ingawa haikuwa rahisi lakini walinielewa,” alisema.

Baadhi ya waumini walisema kwa kuwa mzee Mwingira alikuwa mcha Mungu alipewa maono ya kuandaa mazishi yake.

Kwa kipindi hicho chote cha mwezi mmoja yaliendelea kufanyika maandalizi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa nyumba alikozikwa.

Katika msiba huo hali ilikuwa tofauti na misiba mingine kwani hawakutaka uitwe msiba bali sherehe ya mzee Mwingira.

Watu mbalimbali wakiwamo waumini wa Efatha Ministry walionekana kuvaa sare huku muda mwingi wakiwa wanashangilia. Kwa siku zote 30, mwili huo ulihifadhiwa kwenye Hospitali ya Mashangilio inayomilikiwa na huduma Efatha Ministry iliyopo Kibaha.

Mwili kuagwa

Juzi ilifanyika ibada ya kuaga mwili wa Mzee Elias ambapo watu wa kada mbalimbali walitoa heshima zao za mwisho.

Katika ibada ya maziko viongozi mbalimbali, wakiwemo wanasiasa walitoa heshima za mwisho na salamu za rambirambi.

Wakati wa kuzika hali ilikuwa tofauti na misiba mingine ambapo waliotakiwa kwenda yalipo makaburi ni wanafamilia, viongozi wa dini na kiserikali huku wengine wakibaki kufuatilia matukio ya moja kwa moja kwenye televisheni ya Trinity inayomilikiwa na Efatha.

Yalipofanyika mazishi ni umbali wa zaidi ya mita 800 kutoka eneo lilipo kanisa. Eneo yalikofanyika mazishi liliandaliwa katika muda wote wa mwezi mmoja.