Breaking News

Mwalimu apambania wagombea udiwani wa Chadema Karagwe

Sunday October 18 2020

 

Kagera. Mgombea mwenza wa Urais Chadema Salum Mwalimu amemtaka kamanda wa polisi Wilaya ya Karagwe kumchukulia hatua za kisheria msimamizi msaidizi wa uchaguzi jimbo la Karagwe (Mkurugenzi wa halmashauri) au wagombea udiwani wa chama hicho katikakatika kata za Kayanga na Chanika.

Akihutubia katika mkutano wa Kampeni leo Jumapili Oktoba 18, 2020 mjini Karagwe, Mwalimu amesema kinachoendelea kati ya Mkurugenzi na madiwani hao kinahatarisha usalama na amani katika kata hizo. Hivyo amemuomba mkuu wa Polisi wa Wilaya hiyo achukue hatua kwa upande ambao unahusika na hilo.

“Madiwani hawa wana barua za Tume ya Taifa ya uchaguzi lakini nimeambiwa mkurugenzi wa hapa anawakataza kufanya kampeni kwa kutumia jeshi la polisi, sasa mimi nasema OCD muite mkurugenzi atoe maelezo kwa nini anahatarisha amani, lakini kama viongozi wangu wamefoji barua hizi sio za kweli basi nao wawatie ndani maana nao wanahatarisha amani,”  amesema Mwalimu.

Amesema Mkurugenzi hana mamlaka makubwa kuliko Tume ya Uchaguzi ambayo ilikwishaamua kuhusu wagombea hao hao.

Hivyo wagombea udiwani hao  waendelee na kampeni kama kawaida na endapo watafanyiwa fujo tena watoe taarifa kwa viongozi wa kitaifa wa chama hicho kwa hatua zaidi.

"Katibu wa jimbo andika barua kwa OCD ukimtaarifu juu ya namna mkurugenzi anavyohatarisha amani katika uchaguzi huu, nakala peleka kwa RPC na RAS kisha anzeni kampeni atakayewagusa tupeni taarifa wakati wa mkutano watu wengine wakae pembeni kimkakati mturekodie video ya hao wanaowafanyia fujo mtutumie,” amesema Mwalimu.

Advertisement

Aidha, Mwalimu aliwaita wagombea hao na kuwaombea kura huku akishangiliwa na mamia waliojitokeza kusikiliza mkutano huo, hata hivyo, aliwaeleza kuwa katika kampeni zao endapo kutakuwa na kipigo wasogee kilipo ili wapigwe na ushahidi upatikane vizuri.

Advertisement