VIDEO: NEMC yasema maji ya ‘Kandoro’ yamerejea Dar, yapiga marufuku

Mkurugenzi  wa Nemc,Dk Samuel Gwamaka akizungumza na wanahabari kuhusu uwepo wa maji ya 'Kandoro'

Muktasari:

  • Licha ya Makamu wa Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kupiga marufuku uuzaji wa maji katika mifuko ya plastiki maarufu ‘maji ya Kandoro’, imeelezwa kuwa maji hayo bado yanauzwa maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam.

Dar es Salaam. Licha ya Makamu wa Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kupiga marufuku uuzaji wa maji katika mifuko ya plastiki maarufu ‘maji ya Kandoro’, imeelezwa kuwa maji hayo bado yanauzwa maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam.

Mei, 2019 wakati  akizungumza na watendaji wa mkoa wa Dar es Salaam, Samia alipiga marufuku uuzwaji wa maji hayo kwa maelezo kuwa si salama na kwamba mifuko ya plastiki pia inaharibu mazingira.

Akizungumza leo Jumatano Oktoba 9, 2019 mkurugenzi mkuu wa Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (Nemc), Dk Samuel Gwamaka amesema baada ya wananchi kunywa maji hayo wanatupa mifuko ambayo inaharibu mazingira.

Amesema maofisa wa Nemc 100 waliosambazwa katika maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam kuchukua  takwimu ya hali ya mazingira kwenye makazi ya watu na viwanda ndio imebaini uwepo wa maji hayo.

"Maji haya hayana ubora na hayajathibitishwa na TBS (Shirika la Viwango Tanzania) na makamu wa rais (Samia) alishapiga marufuku matumizi yake. Mifuko ya maji ya Kandoro mtu akitumia anaitupa na kusababisha uharibifu wa mazingira.”

"Ni marufuku kutumia maji haya kwa sababu uzalishaji wake haufuati utaratibu wa TBS. Kwanza hatujui yanatoka wapi na mtengenezaji ni nani, hatuwezi kuruhusu hali hii kama wewe ni muuzaji wa maji haya nenda TBS kafuate utaratibu," amesema Dk Gwamaka.

Mkurugenzi wa sheria wa Nemc, Bernard Kongola amewataka wananchi kuachana na vifungashio hivyo vinayotumika kufungia maji ya Kandoro, akibainisha kuwa faini yake inaanzia Sh 30,000 kwa mujibu kanuni ya 8 ya mwaka 2019 ya  katazo la matumizi ya mifuko ya plastiki.