NLD yaungana na vyama sita kususia uchaguzi serikali za mitaa Tanzania

Muktasari:

Uchaguzi wa Serikali za Mitaa nchini Tanzania umepangwa kufanyika Novemba 24, 2019 huku vyama saba vikiwa vimetangaza kutokushiriki uchaguzi huo.

Dar es Salaam. Chama cha upinzani cha NLD nchini Tanzania kimetangaza kutoshiriki uchaguzi wa serikali za mitaa nchini humo utakaofanyika Novemba 24, 2019.

NLD inaungana na vyama vingine sita kususia uchaguzi huo. Vyama hivyo ni; Chadema, ACT- Wazalendo, UPDP, CUF, Chaumma pamoja na NCCR-Mageuzi.

Taarifa iliyotolewa leo Jumatano Novemba 13, 2019 na Mwenyekiti wa NLD, Oscar Makaidi imesema hawatoshiriki uchaguzi huo kutokana na ukiukwaji wa makusudi wa taratibu, kanuni na sheria ya uchaguzi.

“Tumepokea malalamiko mbalimbali kutoka kwa wagombea wetu zinazothibitisha ukiukwaji na ubakwaji wa demokrasia nchini kwa kiwango cha kutisha kiasi cha kufanya uchaguzi huu kuwa kituko,” amesema Makaidi

“Kwa ujumla uchaguzi umepoteza sifa ya kuitwa uchaguzi,” amesema

Katika taarifa hiyo, Makaidi amesema, “Tunampata waziri mwenye dhamana ya uchaguzi huu- Tamisemi, ndugu Seleman Jafo kujiuzulu mara moja kwa kushindwa kusimamia uchaguzi huu na kulitia taifa hasara.”

“Sisi kama chama hatuna imani naye licha ya kuagiza kuwa wagombea wote walioenguliwa warudishwe, agizo ambalo hana mamlaka nalo kikanuni wala kisheria,” amesema Makaidi mtoto wa aliyekuwa Mwenyekiti wa NLD, Dk Emanuel Makaidi aliyefariki Oktoba 15, 2015.

Makaidi amesema, “kwa kuwa Tamisemi imeshindwa kusimamia uchaguzi huu wa serikali za mitaa, tunataka sasa uchaguzi huu usimamiwe na tume huru ya taifa ya uchaguzi.”

Mwenyekiti huyo, amemalizia taarifa yake kwa kuwataka, “wanachama na wagombea wote nchi nzima kuwa watulivu na kutojihusisha kwa lolote kuhusiana na uchaguzi huu mpaka hapo tutakapo wataarifu vinginevyo.”