NO AGENDA: Kupambana na Masanja ni kupoteza shabaha vita ya corona

Sunday April 5 2020

 

MITANDAONI mastaa Bongo kama nchi ipo tofauti na dunia. Wakati Shirika la Miradi ya Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), linaomba nchi za G20 kutoa dola 2.5 trilioni (Sh5,700 trilioni), kusaidia theluthi mbili ya dunia ambayo ni nchi zinazoendelea, wanaoombewa msaada ni kama hakuna kitu.

Tanzania ni moja ya hizo nchi zenye kuombewa msaada. Janga la virusi vya SARS Corona 2, vinavyosababisha maradhi ya Covid-19, linatetemesha ulimwengu. Nchi za G20 zenyewe zinachapika. Mpaka jana mchana, mtandao wa Worldometers ulionesha waathirika Corana 2 ni zaidi ya 1.1 milioni. Vifo ni 59,491.

Shida kubwa ya Covid-19 sio maambukizi na vifo peke yake. Ni jinsi ambavyo gonjwa hilo linavyosimamisha shughuli za kiuchumi duniani. Jukwaa la Biashara na Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNCTAD), limeshatoa tathmini kuwa kiasi cha dola 2 trilioni (Sh4,600 trilioni), zimeshaondoka kwenye mzunguko wa kifedha duniani tangu Januari mwaka huu kwa sababu ya Covid-19.

Mataifa makubwa yanachapwa mno. China haijapona, Marekani imevamiwa, Italia, Hispania, Uingereza zinashindana kasi ya kuandika rekodi ya vifo vipya. Wapo watu wameanza kuileta nadharia ya mwisho wa dunia (the doomsday theory), kwamba kasi ya mtikisiko wa kiuchumi iliyopo sasa kwa sababu ya Covid-19, inaupeleka ulimwengu kwenye ubashiri wa kikomo chake.

Kwa mujibu wa the doomsday theory, endapo kasi ya ukuaji wa uchumi wa dunia itafikia asilimia 0.5, basi dunia itakuwa inaelekea kugota kwenye ukingo wake. Januari mwaka huu, Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), lilichapisha kwenye jarida la Mtazamo wa Kiuchumi Duniani (World Economic Outlook ‘WEO’) kuwa ukuaji wa uchumi mwaka huu unapaswa kuwa asilimia 3.3, kutoka asilimia 2.9 za mwaka jana.

Dunia imeshikwa pabaya mno. Hakuna nchi iliyo salama. Nguvu kubwa zinaelekezwa kwenye kudhibiti maambukizi. Taifa ambalo litapata maambukizi machache, litaweza kupata nusura kubwa. Wafanyabiashara, wanamichezo, wasanii, viongozi wa dini, wanashikana mikono na Serikali, ujumbe kwa taifa uwe mmoja. Nchi nzima izungumze lugha moja

Advertisement

Adui mkuu ni Covid-19. Kila mwenye elimu ndogo ahakikishe anamfikishia mwenzake ili kusaidiana jinsi ya kujilinda. Watu waelewe Covid-19 ni nini. Wajue inaambukizwaje. Watambue namna bora ya kuishi ili kuwa mbali na maambukizi.

Tukielewa adui mkuu ni nani, hatutaona vishindo vya Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Patrobas Katambi, akitaka msanii wa vichekesho, Emmanuel Mgaya ‘Masanja Mkandamizaji’, ajisalimishe polisi. Eti, kosa ni kuwahoji wananchi wa Dodoma kimasihara kuhusu Covid-19.

Wazo la Katambi ni Masanja ameingiza utani kwenye jambo serious. Ningekuwa Katambi, yale mahojiano ya Masanja na wakazi wa Dodoma, yangenifanya nijue, mosi kuna kazi sijaifanya ipasavyo. Pili, upo wajibu napaswa kuutimiza.

Ningetambua kuwa sijatimiza wajibu wa kuwaelimisha wakazi wa Dodoma kuhusu Covid-19, ndio maana walimjibu kama waliyomjibu. Ningeona kwamba ninao wajibu wa kuhakikisha elimu mahsusi inafika kwa watu.

Kuwahi kumkabili Masanja kwa kuwahoji wakazi wa Dodoma ni kupoteza pointi ya pambano. Jambo la haraka lilikuwa kuwahi kuelimisha watu. Wajue Covid-19 ni nini. Masanja alionesha kuwa watu wanasikia Covid-19 lakini hawajui ni nini, au hawajawahi hata kusikia. Lazima kutazama upya aina ya mfumo wetu wa mawasiliano. Inaonekana walengwa wengi hawapokei ujumbe. Ama wanatengwa au wanajitenga.

Unaingia mitandaoni, msanii maarufu anapost picha ya utani au ya kula bata kufurahia wikiendi. Unajiuliza huyo mtu maarufu anajua dunia ipo kwenye hatari gani? Wakati mwingine usimlaumu yeye, uliza kama ameshaelimishwa ili naye aelimishe wengine.

Duniani, watu maarufu, wasanii na wanamichezo matajiri, wanashindana kutoa michango ya fedha na rasilimali nyingine ili kusaidiana na serikali zao kupambana na Covid-19. Huku, watu wanaonesha fahari ya starehe.

Kuna tukio lingine la takriban wiki moja iliyopita; ilitolewa taarifa na Kamishna wa Polisi, Kanda Maalum Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa, kuwa mtu na mkewe, Boniface na Rosemary Mwita, walishikiliwa na polisi kwa kusambaza taarifa potofu kuhusu Covid-19.

Kwa mujibu wa Mambosasa, wanandoa hao (Mwitas), wakazi wa Tabata, wakiwa kwenye daladala, walisema hapa nchini hakuna Covid-19, bali Serikali inadanganya kusudi ipate misaada.

Mwitas pia inadaiwa walisema Serikali ilitoa tangazo la kufunga shule na vyuo nchi nzima kwa sababu haina fedha za kulisha wanafunzi.

Kwamba kwa kauli zao hizo, abiria wengine kwenye daladala waliagiza gari lipelekwe kituo cha polisi, Mwitas wakaripotiwa na kushikiliwa.

TUNAPOTEZA SHABAHA

Vita kuu ya nchi kwa sasa ni mapambano dhidi ya Covid-19. Nguvu kubwa inapaswa kuelekezwa katika kulinda watu ili maambukizi yasisambae zaidi.

Ulinzi wa watu ni pamoja na kuelimishana. Wasio na taarifa sahihi wazipate ili nao wakaelimishe wengine.

Yupo mtu atasema Mwitas ni vidomodomo, kwangu naona hawana ufahamu kuhusu Covid-19 na hatari zake. Wanapaswa kuelimishwa. Wakishaelimika, wataelimisha na wengine. Hivyo ndivyo tutaishinda Corona.

Huu si wakati wa kunyooshana. Bali tuunganishe nguvu kuinyoosha Covid-19. Tukitumia nguvu nyingi kunyooshana, tutashituka Covid-19 imetunyoosha.

Sioni mantiki ya Mambosasa kutoa taarifa ya Mwitas kwenye vyombo vya habari kwamba wanawashikilia, badala yake walitakiwa kuonywa, kuelimishwa na kuachiwa kimyakimya ili nao wakaelimishe wengine.

Duniani kwa sasa, nchi mbalimbali zinaachia wafungwa wenye makosa madogo na ambao wanakaribia kumaliza vifungo. Sisi huku ndio kwanza tunakamata watu.

Supastaa wa Hollywood, Harvey Weinstein, ambaye ni mfungwa wa ubakaji, amepata Covid-19 gerezani. UN wanasema Covid-19 inasambaa magerezani na wafungwa 8,000 wameachiwa Iran.

Kamishna wa Haki za Binadamu wa UN, Michelle Bachelet, ametaka wafungwa waachiwe ili kudhibibiti Covid-19. Sisi tunataka waongezeke.

Tuachane na vita ndogo. Mwitas na Masanja sio vita yetu. Adui mkuu ni Covid-19. Wapotoshaji waelimishwe, kisha tusimame pamoja kama jeshi moja dhidi ya Covid-19.

Katika hili la Covid-19, kila Mtanzania ni mdau. Tushirikiane kama taifa. Tuhakikishe hakuna aliye nyuma. Tusambaziane elimu. Kwa pamoja tuta-shinda.

Advertisement