Nape adai viongozi vyama vya ushirika mikoa ya kusini wanatishiwa

Mbunge wa Jimbo la Mtama Nape Nnauye akiuliza swali bungeni leo wakati wa Mkutano wa kumi na saba kikao cha saba. Picha na Anthony Siame

Muktasari:

Mbunge wa Mtama (CCM), Nape Nnauye amesema uhaba wa magunia kwa ajili ya kuhifadhi korosho umewafanya viongozi wa ushirika kutishiwa maisha na wengine kufungiwa kwenye ofisi.

Dodoma. Mbunge wa Mtama (CCM), Nape Nnauye amesema uhaba wa magunia kwa ajili ya kuhifadhi korosho umewafanya viongozi wa ushirika kutishiwa maisha na wengine kufungiwa kwenye ofisi.

“Tangu msimu umeanza (wa korosho) upatikanaji wa magunia ni mbaya sana. Leo asubuhi viongozi wa vyama vya ushirika wanatishiwa maisha wengine wanafungiwa kwenye ofisi.”

“Wakulima wanapatiwa magunia mawili.  Serikali inatoa tamko gani kuokoa hali hiyo,” amehoji Nape bungeni mjini Dodoma leo Jumanne Novemba 12, 2019 wakati akiuliza swali la nyongeza.

Akijibu swali hilo naibu Waziri wa Kilimo, Omary Mgumba amesema kuna changamoto  ya magunia na Serikali imeona.

“Wenye jukumu la kuagiza magunia ni vyama vya ushirika, hao ndio waliagiza lakini baada ya kusuasua tumeingilia kati na kuongea na msambazaji,” amesema.

Mgumba amesema hadi sasa magunia milioni 2.4 yapo bandarini na hadi leo saa 4:00 asubuhi yameshatolewa magunia 700,000.

Amesema jana yalipakiwa magunia 250,000 kwa ajili ya kupelekwa mikoa ya kusini na leo yamepelekwa magunia mengine 255,000.