Ndugai amueleza Dk Shoo ugumu wa kuwa Spika

Thursday May 9 2019

Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai 

By Aurea Simtowe, mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai amesema watu wanapaswa kujua ugumu wa kuwa na wadhifa huo na kuwataka wajifunze kuchuja baadhi ya maneno yanayowekwa katika mitandao ya kijamii kwa sababu mengi si ya kweli.

Ameyasema hayo leo Alhamisi Mei 9, 2019 katika ibada ya mazishi ya aliyekuwa mwenyekiti wa Kampuni za IPP, Reginald Mengi iliyofanyika katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) usharika wa Moshi mjini mkoani Kilimanjaro.

Amesema wakati watu wakisema katika mitandao ya kijamii ni lazima wajue kazi ngumu aliyonayo.

“Nafikiri baba Askofu (Dk Fredrick Shoo- mkuu wa KKKT) umeona ugumu wa kuwa spika, umejaribu tu kidogo umeona wewe mwenyewe shughuli iliyotokea.”

“Kwa hiyo mnaposema kwenye mitandao ya kijamii kuhusu Ndugai mjue kazi ngumu niliyonayo,” amesema Ndugai.

Akizungumzia tabia ya baadhi ya watu kumuandika vibaya Mengi amesema hata wao hukumbwa na mambo hayo akiwataka watu kutoamini kila kinachoandikwa katika mitandao hiyo.

Advertisement

“Ujumbe huu ni kwa Watanzania na kwa baba zetu wapaka mafuta wa bwana siyo vyote mnavyovisoma ni kweli, ni vizuri pale ambapo mna mashaka kidogo basi mkatuuliza.”

“Sisi ni wenzenu, Watanzania wenzenu, tumekulia humu humu Moshi sasa tunageukaje tunakuwa watu wa ajabu haiwezekani,” amesema Ndugai.

 

 

Advertisement