Njia, vituo vya daladala jijini Mwanza vyabadilishwa

Monday February 17 2020

 

By Mgongo Kaitira, Mwananchi [email protected]

Mwanza. Jiji la Mwanza limetangaza mabadiliko ya njia za daladala na vituo vya kupakia na kushusha abiria katikati ya Jiji.

Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya jiji la Mwanza, Kiomoni Kibamba amelieleza Mwananchi leo Jumatatu Februari 17, 2020 kwamba mabadiliko hayo yameanza Februari 15, 2020.

Amesema yanalenga kuondoa msongamano katikati ya mji, hasa eneo la barabara ya Pamba ambako unaendelea ujenzi wa soko kuu jipya.

“Tunataka kusiwepo msongamano wa daladala zinazosimama kupakia na kushusha katika barabara ya Pamba ili kurahisisha utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa soko kuu unaotarajiwa kuanza wakati wowote,” amesema Kibamba.

Miongoni wa njia zilizobadilishwa vituo vya kupakia na kushusha abiria ni Buhongwa - Nyegezi – Igoma - Kishiri, Buhongwa - Nyegezi - Igoma – Kisesa na Uwanja wa Ndege – Igoma – Kisesa.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Chama cha Madereva na Makondakta wa Daladala mkoa wa Mwanza (Mwaredda), Mjalifu Manyasi Mkoa huo unakadiriwa kuwa na daladala zaidi ya 3, 000, kati ya hizo zaidi ya 800 huingia na kutoka katikati ya Jiji.

Advertisement

Ili kuwezesha umma kutambua mabadiliko hayo ya njia, Halmashauri ya Jiji kwa kushirikiana na wadau wengine wa sekta ya usafirishaji jijini Mwanza wamebandika matangazo katika nguzo na kuta mbalimbali huku gari la matangazo ya umma pia likipita mitaani kutoa matangazo.

Advertisement