Ofisi ya serikali Moshi yachomwa moto wa petroli

Moshi. Nani wamehusika? hili ndilo swali linawaumiza vichwa wapelelezi baada ya watu wasiojulikana kuchoma moto ofisi ya Serikali ya mtendaji wa kata ya Soweto katika Manispaa ya Moshi.

Tukio hilo limetokea wakati mchakato wa uchaguzi wa serikali za mitaa ambao umekumbwa na utata ukiendelea, lakini baadhi ya watu wamelihusisha na uhalifu wa kawaida.

Taarifa kutoka eneo la tukio zinaeleza kuwa watu hao walichoma ofisi hiyo kwa kutumia mafuta ya petroli na kusababisha baadhi ya nyaraka na samani za ofisi kuungua.

Tayari watu kadhaa wanashikiliwa na polisi, akiwamo Collin Myuta ambaye ni diwani wa Kata ya Soweto (Chadema), huku chama hicho kikitaka weledi katika uchunguzi wa tukio hilo. Katibu wa Chadema mkoani Kilimanjaro, Basil Lema alisema haelewi sababu za polisi kumhusisha diwani wao na tukio hilo na kufanya lionekane ni tukio lenye sura ya kisiasa kuliko jinai.

Alisema ni mapema mno kulihusisha suala hilo na siasa na hawaelewi sababu za diwani huyo kukamatwa.

Hata hivyo, kamanda wa polisi wa mkoa, Salum Hamdani alisema hawajasema kama diwani huyo na wengine wamehusika bali wanashukiwa.

“Jukumu letu ni kuchunguza na kuwapata watu wote waliohusika kwa namna moja ama nyingine na kuchoma hiyo ofisi. Suala la mtu kukamatwa halina limitation (mipaka),” alisema Hamdani.

“Sisi tumekamata watu kadhaa ambao tunawashuku kuwa huenda wamejihusisha kwa namna moja ama nyingine na tukio hilo. Hatujasema wamehusika. Tunawatuhumu kuwa wamehusika,” alisema.

“Tunaendelea na taratibu za mahojiano na watapewa haki zao za msingi kulingana na sheria. Tunaendelea na upelelezi ila kuna watu kadhaa tunawashikilia akiwamo huyo diwani,” alisema.

Tukio lilivyokuwa

Taarifa iliyotolewa jana na Shaban Pazi kwa niaba ya Katibu Tawala wa Mkoa (RAS), inasema usiku wa kumkia jana, jirani anayeishi karibu na ofisi hiyo alihisi harufu ya moshi.

“Harufu ya moshi iliyochanganyika na mafuta ya petroli ilimshitua mkazi mmoja anayeishi jirani na ofisi hiyo ambaye alichungulia nje na kuona jengo la ofisi ya kata likiungua,” alisema.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mkazi huyo aliwaamsha majirani na kwa kushirikiana na kikosi cha doria cha kata hiyo, walifanikiwa kuuzima moto ulioanzia madirisha ya mbele.

Taarifa hiyo inasema uchunguzi wa awali umebaini kuwa moto huo uliwashwa kwa makusudi kupitia madirisha ya mbele ya jengo hilo ambayo yanaonyesha yalimwagiwa mafuta na kuwashwa.

“Wahalifu hao walitelekeza kiberiti ambacho kimeonekana kikiwa na njiti pamoja na msokoto wa bangi. Moto huo umeunguza sehemu ndogo ya jengo na nyaraka zilizokuwa jirani,” inasema.

Miongoni mwa nyaraka hizo ni taarifa za chanjo, machapisho na makabrasha ya afya na kutokana na tukio hilo, mkuu wa mkoa, Anna Mghwira amewataka wananchi kuwa watulivu.

Mghwira ameagiza vyombo vyote vya ulinzi na usalama kuwa macho na vitendo vyote vya uhalifu vyenye nia ya kuvuruga amani na usalama katika mkoa huo.

Tukio hilo limekuja kukiwa na taarifa pia za kukatwa kwa mazao katika shamba la msimamizi msaidizi wa uchaguzi wilayani Chunya mkoa wa Mbeya, tukio linalohusishwa na chuki za kisiasa.

Tayari Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, Inspekta Jeneral wa Polisi (IGP), Simon Sirro na Mkurugenzi wa Upelelezi (DCI), Robert Boazi, wameonya watu ambao wamedai wanahamasisha vurugu.

Maagizo hayo yanatokana na baadhi ya watu wakiwamo wanasiasa, kutangaza kutoshirikiana na CCM na wagombea wote wa chama hicho walioenguliwa na wasimamizi.

Vyama takriban vinne vikubwa vimetangaza kujitoa katika uchaguzi huo, zikilalamikia vitendo vya wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi kama kutoshinda ofisini kusubiri warejeshe fomu.