Papa Msofe na wenzake kortini wakidaiwa utakatishaji fedha

Monday December 2 2019

 

By Hadija Jumanne, Mwananchi. [email protected]

Dar es Salaam. Mfanyabiashara, Marijan Msofe, maarufu kama ‘Papa Msofe’ na wenzake wanne, wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakikabiliwa na mashtaka matano likiwemo la kujipatia fedha kiasi cha Sh943 milioni kwa njia ya udanganyifu.

Hata hivyo, si mara ya kwanza kwa Papaa Msofe kufikishwa mahakamani hapo, kwa sababu aliwahi kukabiliwa na kesi ya Mauaji mwaka 2012 na baadaye  alifunguliwa kesi ya kughushi mwaka 2015.

Mbali na Msofe, washtakiwa wengine ni

wakili wa kujitegemea, Mwesigwa Mhingo, Wenceslau Mtui, Josephine Haule na Fadhil Mganga.

Miongoni mwa mashtaka yanayowakabili ni kuratibu genge la uhalifu, utakatishaji fedha na kujipatia fedha kwa Njia ya udanganyifu.

Washtakiwa hao wamefikishwa mahakamani hapo leo, Desemba 2, 2019 na kusomewa mashtaka yao mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Huruma Shaidi.

Advertisement

Akiwasomea hati ya mashtaka, wakili wa Serikali Mwandamizi, Ladislaus Komanya, ameieleza mahakama hiyo kuwa washtakiwa wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi namba 124/2019

 

Wakili Komanya amedai kuwa washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa kutenda makosa hayo kati ya Desemba 2018 na Septemba 2019 katika maeneo tofauti ya jiji la Dar es Salaam, ambapo wanadaiwa kuwa walifanya mpango wa kutekeleza kosa la kijinai.

Komanya amedai katika  kosa la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, washtakiwa wanadaiwa kutenda kosa hilo  kati ya Desemba 2018 na Septemba 2019, Jiji la Dar es Salaam ambapo wakiwa na nia hiyo walijipatia Dola za Kimarekani 300,000 (Sawa na Sh660 milioni) kutoka kwa Pascal Camille wakidai ni pesa za kuumuzia madini ya dhahabu kilo 200 ambayo wangemsafirishia kwenda Ureno wakati wakijua si kweli.

Vilevile, wanadaiwa  kati ya tarehe hizo hizo, walimlaghai Johnson Mason kwamba watamuuzia kilo 20 za madini ya dhahabu yenye thamani ya Sh 253milioni na wangemsafirishia kwenda nchini Ureno wakati wakijua si kweli.

Katika shtaka la kutakatisha fedha, washtakiwa hao wanadaiwa, kati ya Desemba 2018 na Septemba 2019 katika maeneo mbalimbali jijini Dar es , washtakiwa wanadaiwa kutakatisha  dola 300,000, sawa na Sh690 milioni kutoka kwa  Pasco Camile, wakati akijua ni zao la udanganyifu.

Katika shtaka la na tano  ni kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu inadaiwa siku hiyo kwa njia ya udanganyifu walijipatia kiasi Sh 253milioni  kutoka kwa John Mahsson kwa kumdanganya kuwa watamuuzia dhahabu na kisha kuzisafirisha kwenda nchini Ureno.

Washtakiwa baada ya kusomewa mashtaka yao, hawakurusiwa kujibu chochote kwa sababu mashtaka yanaowakabili ni uhujumu uchumi.

Upande wa mashtaka ulidai kuwa  upelelezi wa shauri hilo  bado haujakamilika na kuomba tarehe nyingine ya kutajwa.

Hakimu Shaidi aliahirisha kesi hiyo Desemba 16, 2019, itakapotajwa na washtakiwa wamerudishwa rumande.

Msofe na wenzake wapandishwa kizimbani wakidaiwa kutakatisha Sh943 milioni, hata hivyo, si mara ya kwanza kwa Msofe kufikishwa mahakama hapo, kwa sababu aliwahi kukabiliwa na kesi ya mauaji mwaka 2012 na baadaye  alifunguliwa kesi ya kughushi mwaka 2015.

Advertisement