Polepole awapa somo vijana CCM kabla hawajawa viongozi

Muktasari:

  • Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) nchini Tanzania, Humphrey Polepole ameendesha darasa la itikadi kwa wanafunzi wa shirikisho la vijana wa CCM wa vyuo vikuu na kati jijini Arusha.

Arusha. Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) nchini Tanzania, Humphrey Polepole amewataka vijana kujenga tabia ya kujijenga kwa kujitolea mambo ya kijamii kabla kuja kugombea uongozi

Polepole amesema hayo leo Jumapili Februari 9, 2020 katika darasa la shirikisho la vijana wa CCM wa vyuo vikuu na kati jijini Arusha.

Amesema vijana wasisubirie kuwa viongozi ndio watoe michango yao katika jamii kwani atakuwa anaharibu mwonekano na taswira ya kuwa kiongozi kwa watu utakaowaongoza.

"Vijana mnapaswa  kujiandaa katika utumishi na uongozi kwa jamii nakuleta maendeleo kabla ya kugombea ili kuweza kuwashawishi watu utakaowaongoza katika jamii inayokuzunguka na hii ni moja ya sifa itakayowasaidia kuwa kiongozi kwa wananchi kukuchagua," amesema Polepole.

Amesema ni vyema vijana wakaanza sasa kutatua changamoto katika jamii na wasisubiri hadi wawe viongozi ndio wafanye hayo kwani watakuwa wanajipunguzia sifa ya kuwaongoza wananchi na wakashindwa kukuchagua kwa kukosa sifa ya utumishi kabla ya kuhitaji uongozi.

Polepole amesema vijana wajenge tabia ya kusoma vitabu mbalimbali na magazeti ili kuwaongezea maarifa ya kujua vitu mbalimbali.