Polisi Tanzania yamsaka Zitto Kabwe

Muktasari:

Kiongozi wa chama cha upinzani nchini Tanzania cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe anatafutwa na Polisi nchini humo kwa mahojiano baada ya mkutano wake na waandishi wa habari uliokuwa ufanyike kugonga mwamba.

Dar es Salaam. Polisi mkoa wa Kinondoni nchini Tanzania imesema inamtafuta Kiongozi wa chama cha upinzani nchini humo cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe kwa ajili ya mahojiano.

Kamanda wa Polisi huo, Mussa Taibu akizungumza na Mwananchi leo Ijumaa Agosti 16,2019 amesema baada ya polisi kuzuia mkutano wa kiongozi huyo na waandishi wa habari uliokuwa ufanyike mapema leo asubuhi.

Baada ya polisi kuzuia mkutano huo uliokuwa unatarajiwa kufanyikia makao makuu ya chama hicho Kijitonyama jijini Dar es Salaam, polisi walimshikilia kwa muda mfupi Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mawasiliano wa chama hicho, Ado Shaibu kabla ya kumwachia huru.

Kamanda Taibu amesema polisi mkoa wa Kinondoni hawajamkamata mtu yoyote wala kuzuia mkutano kati ya  chama hicho na waandishi wa habari bali wanamuhitaji Zitto kwa ajili ya mahojiano.

Ameongeza hana shida na msaidizi huyo wa Zitto (Shaibu) bali wanamhitaji Zitto mwenyewe. Hata hivyo, kamanda huyo hakueleza mahojiano hayo yanahusu nini au kosa gani alilotenda.

“Mimi sina shida na msaidizi wake bali namuhitaji Zitto Kabwe aje hapa ofisini kwa ajili ya mahojiano. Narudia kusema sijamkamata mtu yoyote, huyo ambaye polisi walimchukua siyo ambaye nilikuwa namuhitaji,” amesema Taibu.

Zitto alipanga kuzungumza na vyombo vya habari kuhusu Mkutano wa 39 wa Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) unaofanyika Tanzania kwa sababu polisi walivamia ofisi za chama hicho na kuwataka waandishi wa habari waliokuwepo hapo kutawanyika.

Polisi hao waliwasili katika ofisi za ACT Wazalendo saa 4:45 asubuhi na gari lenye namba za usajili T863 DFS wakiwa wamevaa nguo za kiraia na kuzuia mkutano huo. Baadaye gari ya polisi walio na sare waliwasili na kumhitaji kiongozi yoyote wa chama baada ya kumkosa Zitto.

“Ndugu waandishi huu mkutano usubiri kwanza, kwa hiyo ninawaomba mtawanyike mara moja,” alisema askari mmoja aliyejitambulisha kama RCO wa Kinondoni, John Malulu.

Wakati waandishi wakitawanyika, Shaibu aliwasili kwenye ofisi za chama hicho na kutakiwa kuondoka na polisi. Shaibu alitii agizo hilo na kuondoka na askari hao mpaka kituo cha polisi cha Oysterbay.

Hata hivyo, kabla ya kuchukuliwa na polisi, Ado Shaibu alisema alikuwa na taarifa kwamba polisi walikwenda nyumba kwa Zitto kumtafuta kwa ajili ya kumhoji hayo lakini walimkosa.

“Zitto alitaka kuzungumzia mkutano wa Sadc unaondelea hapa nchini lakini wameniambia niondoke nao kwenda polisi, hawajaniambia ni kituo gani. Nimewaambia ngoja niweke mambo sawa kisha tuondoke. Hamna haja ya kuwa na wasiwasi, mapambano lazima yaendelee,” alisema Shaibu.

Alipotafutwa kuzungumzia wito huo wa polisi, Zitto hakuweza kupatikana mara moja kuzungumzia suala hilo na jitihada za kumtafuta zinaendelea.

Endelea kufuatilia Mwananchi kwa habari zaidi