Profesa Kabudi abainisha uzembe matumizi ya Kiswahili Afrika Kusini

Muktasari:

 Rais wa Tanzania, John Magufuli amewaapisha mabozi wanne watakaokwenda kuiwakilisha nchi hiyo katika mataifa mbalimbali. Shughuli ya kuapisha imefanyika Ikulu Dar es Salaam.

Dar es Salaam. Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki nchini Tanzania, Profesa Palamagamba Kabudi amesema Tanzania ilizembea kupata fursa ya kufundisha lugha ya Kiswahili nchini Afrika Kusini na kusababisha fursa hiyo kuangukia kwenye nchi nyingine.

Akizungumza katika hafla ya kuwaapisha mabalozi wanne Ikulu ya Dar es Salaam leo Jumanne Januari 14, 2020 Profesa Kabudi amesema kutokana na juhudi za Rais John Magufuli aliyefanya ziara nchini humo mwaka 2019 ndipo fursa hiyo ikapatikana.

Amemtaka Balozi mpya atakayeiwakilisha Tanzania nchini humo, Meja Jenerali Gaudence Milanzi kutoipoteza tena fursa hiyo.

“Naomba nitembee nuruni na msema kweli ni mpenzi wa Mungu. Fursa hiyo ilikuwa imetuteleza na ilikuwa imeangukia mahali ambapo kwa hadhara hii nisiiseme lakini mmoja anaifahamu,” amesema Profesa Kabudi.

“Isingekuwa juhudi binafsi za Rais alipokutana na Rais wa Afrika Kusini bahati hiyo ilikuwa imetupita. Ni we mkweli, fursa hiyo ilikuwa imetupita si kwa sababu yoyote ile bali ni uzembe wetu wenyewe.”

Amesema kwa sasa lugha ya Kiswahili inafahamika na watu wengi nchini humo lakini walimu wanaotumiwa ni kutoka nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Amemtaka Meja Jenerali Milanzi kumtafuta Waziri wa Basic Education (elimu ya msingi) wa Afrika Kusini ili jambo hilo likamilishwe kabla ya Februari.

“Ili juhudi binafsi za Rais alipokutana na Rais Cyril Ramaphosa zisipotee. Tusifanye makosa mara ya pili kuipoteza fursa hiyo. Itakuwa muhali,” amesema.

Amemtaka pia kufuatilia mambo yaliyokubaliwa kati ya Rais Ramaphosa alipokuja Tanzania na na kukutana na Rais Magufuli, likiwamo suala la ushirikiano kati ya shule ya msingi ya Chief Albert Luthuli Mazimbu (Morogoro) na shule za Afrika Kusini.

Mabalozi walioapishwa ni Meja Jenerali Gaudence Milanzi anayekwenda nchini Afrika Kusini, Dk Modestus Kipilimba anayekwenda kufungua ubalozi nchini Namibia, Mchungaji Profesa Emmanuel David Ubalozi anayekwenda nchini Zimbabwe na Dk Benson Bana anayekwenda nchini Nigeria na kuwakilisha vituo vingine 16 vya nchi za Magharibi.