Profesa Kabudi asema Nyerere amegoma kufa

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki nchini Tanzania, Profesa Palamagamba Kabudi

Muktasari:

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki nchini Tanzania, Profesa Palamagamba Kabudi amesema licha ya mwalimu Julius Nyerere kufariki dunia, amegoma kufa kwa kuwa misingi yake bado inaishi.

Dar es Salaam. Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki nchini Tanzania, Profesa Palamagamba Kabudi amesema licha ya mwalimu Julius Nyerere kufariki dunia, amegoma kufa kwa kuwa misingi yake bado inaishi.

Ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Oktoba 10, 2019 katika kongamano la kumbukizi ya Rais huyo wa kwanza wa Tanzania lililofanyika Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM). Nyerere alifariki dunia London, Uingereza Oktoba 14, 1999

Profesa Kabudi amesema viongozi waliopewa dhamana ya uongozi wana deni la kuishi misingi  ya mwalimu Nyerere kwa sababu licha ya kutokuwepo hotuba zake zinasikika kila siku.

"Ingawa Nyerere haonekani amegoma kufa na sisi tunakubali amefariki  lakini tunagoma kuwa amekufa, anaendelea kusimamia misingi ya nchi hii," amesema Profesa Kabudi.

Profesa Kabudi ambaye amemwakilisha Rais John Magufuli katika kongamano hilo alitaja baadhi ya mambo aliyoanzisha kiongozi huyo ambayo Serikali ya Awamu ya Tano inaendeleza kuwa ni makao makuu ya nchi kuwa Dodoma na ujenzi wa mradi wa umeme wa mto Rufiji.

“Wote tumehamia Dodoma na alipoona dalili ya kurudi alifuta posho, ukiwa Dar es Salaam hakuna posho na kule hakuna aliyekosa nyumba ya kuishi," amesema Profesa Kabudi.

Awali makamu mkuu wa UDSM, Profesa  William Anangisye  amesema kongamano hilo linajikita kuchambua na kutathmini juhudi za kuendeleza misimamo ya kifalsafa iliyokuwa misingi na maisha ya mwalimu Nyerere.

Kongamano hilo limeandaliwa na Kigoda cha Mwalimu Nyerere cha Taaluma za Umajumui kwa ushirikiano na Chuo cha Uongozi.