RC Gambo apiga marufuku video za miundombinu iliyoharibika kusambazwa

Muktasari:

Mkuu wa Mkoa wa Arusha,  Mrisho Gambo amepiga marufuku waongoza utalii wanaofanya shughuli zao mkoani Arusha  kusambaza picha za video zinazoonyesha miundombinu iliyoharibika katika  mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro.

 

Arusha. Mkuu wa Mkoa wa Arusha,  Mrisho Gambo amepiga marufuku waongoza utalii wanaofanya shughuli zao mkoani Arusha  kusambaza picha za video zinazoonyesha miundombinu iliyoharibika katika  mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro.

Ametoa onyo hilo leo Jumapili Februari 16, 2020 baada ya kutembelea eneo hilo na kushuhudia ubovu wa barabara uliotokana na mvua zinazoendelea kunyesha maeneo mbalimbali.

“Ni marufuku kwa mtu yoyote kusambaza taarifa kuhusu hifadhi zetu bila kupata kibali cha mamlaka husika, kwetu  huu ni uhujumu uchumi kwani tunazitegemea sana hifadhi hizi kwa kuliingizia kipato Taifa,” amesema.

Amesema kama kuna changamoto yoyote mtu ameona anapaswa kutoa taarifa katika mamlaka husika na si katika mitandao ya kijamii.

Gambo amelitaka Jeshi la Polisi mkoani humo kwa kushirikiana na vyombo vingine kama Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kuhakikisha wanawasaka waliosambaza video na picha zenye lengo la kuchafua taswira ya hifadhi

“Wakamatwe ili watueleze malengo yao ni nini kama sio kutufukuzia watalii wetu jambo ambalo kwa mtizamo wangu naliona kama ni uhujumu uchumu,” amesema.

Katika ziara hiyo Gambo ameeleza kuridhishwa na hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Mamlaka ya Ngorongoro katika kukabiliana na changamoto hiyo.