Rais Magufuli: Sitaongeza muda wa uongozi

Muktasari:

Rais wa Tanzania, John Magufuli amesema atazingatia sheria na katiba na hategemei kuongeza hata siku moja muda wake wa uongozi ukiisha.

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, John Magufuli amesema hategemei kuongeza hata siku moja akishamaliza muda wake wa uongozi.

Mkuu huyo wa nchi ametoa msisitizo huo leo Jumatano Desemba 18, 2019 wakati anazindua mradi wa Visima vya maji Chato na kuzungumza na wananchi wilaya hiyo katika uwanja wa Shule ya Msingi Chato mkoani Geita.

“Ndio maana nimekuwa nikisisitiza, nitazingatia sheria na katiba na kwamba sitegemei kuongeza hata siku moja nikishamaliza muda wangu, narudia tena sitegemei kuongeza hata siku moja baada ya kumaliza muda wangu” amesisitiza Rais Magufuli

Amesema muda ulipo kwa mujibu na katiba ndio muda ambao amepewa na Mungu kuwatumikia Watanzania

“Kwa sababu muda nitakaoumaliza kwa mujibu wa katiba ndio muda nitakaokuwa nimepewa na mwenyezi Mungu wa kuwatumikia Watanzania” amebainisha mkuu huyo wa nchi nakuongeza

“Nimeona nilizungumze hili kwa uwazi kabisa ili wale wanaofikiria fikiria kuongeza ongeza, yale mawazo yawe yanawatoka, Watanzania milioni 55 kila mmoja anaweza” amesema

Rais Magufuli aliingia madarakani Novemba 5, 2015 na muhula wa miaka mitano utamalizika mwaka 2020 na mitano ya mwisho endapo atachaguliwa tena mwakani itahitimishwa mwaka 2025.