Rais Magufuli aagiza hospitali kujengwa wilayani Ubungo

Muktasari:

Rais wa Tanzania, John Magufuli leo Jumamosi  Oktoba 26, 2019 amemtaka Waziri wa Tamisemi, Seleman Jafo  kutafuta Sh1.5 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa hospitali ya Wilaya ya Ubungo, jijini Dar es Salaam.

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, John Magufuli leo Jumamosi  Oktoba 26, 2019 amemtaka Waziri wa Tamisemi, Seleman Jafo  kutafuta Sh1.5 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa hospitali ya Wilaya ya Ubungo, jijini Dar es Salaam.

Rais Magufuli ametoa agizo hilo leo katika mapokezi ya ndege mpya aina ya Boeing 787-800 Dreamliner  kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) baada ya kuombwa na mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda.

“Kwanza nimefurahi sana Makonda umeomba hospitali ya wilaya Ubungo na umeomba Sh1.5 bilioni,  nitazitoa ujenge hospitali. Hatuwezi kuacha wananchi wa Ubungo wateseke wakitaka kutibiwa waende mpaka wilaya nyingine, hapana, tutajenga hospitali nyingine.”

“Waziri wa Tamisemi uko wapi? (huku akiangaza walipokuwa wameketi viongozi). Tafuta hela ujenge hospitali ya Ubungo,” amesema Magufuli.

Awali, Makonda aliwataja wabunge wa upinzani jijini Dar es Salaam; John Mnyika (Kibamba), Saed Kubenea (Ubungo) na Halima Mdee (Kawe), akibainisha kuwa hawashiriki shughuli za maendeleo, kumuomba Rais Magufuli kumsaidia kiasi hicho cha fedha kwa ajili ya ujenzi wa hospitali hiyo.