VIDEO: Rais Magufuli ataja sababu kusitishwa kwa miradi

Muktasari:

Rais  wa Tanzania, John Magufuli  amefichua siri ya kusitishwa kwa baadhi ya miradi ya kimkakati ikiwemo ujenzi wa stendi mpya ya Nzega mkoani Tabora, Nyegezi mkoani Mwanza pamoja na soko huu.

Mwanza. Rais  wa Tanzania, John Magufuli  amefichua siri ya kusitishwa kwa baadhi ya miradi ya kimkakati ikiwemo ujenzi wa stendi mpya ya Nzega mkoani Tabora, Nyegezi mkoani Mwanza pamoja na soko huu.

Akizungumza na wananchi wa Nzega akiwa njiani kwenda mkoani Shinyanga leo Jumatano Novemba 27, 2019, Rais Magufuli amesema fedha zilizopangwa kutekeleza miradi hiyo pamoja na mengine katika wilaya na mikoa kadhaa nchini zimepelekwa kwenye miradi mingine yenye faida na maslahi zaidi.

“Siyo stendi ya Nzega pekee hata ile ya Nyegezi Mwanza pia. Mwanza walipanga kujenga soko kuu jipya la kisasa lenye ghorofa, sijui utauza nyanya kwenye ghorofa? Tumesitisha na kuhamishia fedha kwenye miradi mingine yenye faida na maslahi zaidi,” amesema Rais Magufuli.

Jiji la Mwanza lilipanga kutekeleza mradi wa ujenzi wa soko jipya la kisasa la ghorofa mbili lenye vyumba 500 na vizimba 1,500 kwa ajili ya wafanyabiashara wadogo pamoja na eneo la kuegeshea magari zaidi ya 500. Mradi huo ungegharimu zaidi ya Sh23 bilioni.

Kwa mujibu wa mkurugenzi wa jiji la Mwanza, Kiomoni Kibamba mradi wa stendi mpya la Nyegezi ulitengewa Sh14 bilioni.

Stendi ya kisasa la Nyegezi nayo ingekuwa na jengo la ghorofa  mbili  lililopangwa kutumika kwa ajili ya shughuli mbalimbali ikiwemo ofisi ya kampuni ya mabasi na maeneo ya biashara.

Jiji la Mwanza pia lilipanga kutumia zaidi ya Sh13 bilioni kutekeleza mradi wa ujenzi wa maegesho ya magari makubwa ya mizigo eneo la Buhongwa.

Miradi yote mitatu ambayo ni kati ya miradi kadhaa ya kimkakati nchini iliyositishwa na Serikali hadi taarifa nyingine itakapotolewa ilipangwa kuanza  Agosti, 2019 na kukamilika baada ya miezi 18.